Na Elinipa Lupembe.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), wilaya ya Arumeru, imeweka mikakati ya ukusanyaji wa mapato ya halmashauri za wilaya hiyo za Arusha na Meru, lengo likiwa kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya serikali pamoja na kuzuia mianya ya upotevu wa mapato.
Mikakati hiyo imebainishwa na Kamanda Mkuu wa TAKUKURU wilaya ya Arumeru, Deo Mtui, wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha watalamu, wakusanya mapato na Mawakala wa mapato wa halmashauri mbili za wilaya hiyo, kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano chuo cha Ualimu Patandi.
Kamanda huyo amesema kuwa TAKUKURU imefuatilia na kuchunguza hali ya ukusanyaji wa mapato na kubaini changamoto za mashine za kielektroniki za kukusanyia mapato 'POS', ambazo zinaweza kusababisha upotevu wa mapato ikiwemo, wakusanya mapato kutokuweka fedha benki kwa wakati mara baada ya kukusanya na utaratibu hafifu wa ukusanyaji wa ushuru hasa kwenye minada ya mifugo.
"Tunalazimika kuwa na mkakati wa kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato lakini zaidi kuthibiti upotevu wa mapato hayo, kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za ukusanyaji ikiwemo uwasilishaji wa fedha za Umma kwa wakati, kinyume na hapo ni uvunjifu wa sheria, unaobainisha viashiria vya rushwa"Amefafanu Mtui
Hata hivyo Kamanda huyo wa TAKUKURU amewataka Mawakala wa makusanyo ambao wanadaiwa fedha walizokusanya, kuhakikisha wanaweka fedha hizo kwenye akaunti za halmashauri kabla ya kufikia tarehe 05.10.2022 na kuwaagiza wakurugenzi wa halmashauri hizo kusimamia zoezi hilo ili fedha hizo za serikali ziwe mahali sahihi tayari kwa matumizi ya kuwahudumia wananchi.
Awali wakurugenzi wa halmashauri zote mbili, wameahidi kufanyia kazi maoni na ushauri sambamba na kutekeleza maagizo ya kuimarisha usimamaizi wa ukusanaji mapato huku wakifuatilia wadaiwa sugu ambao hawajaweka fedha hizo kwenye akaunti za halmashauri ifikapo tarehe 05, Oktoba.
Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi, amebainisha umuhimu wa kikao kazi hicho, kilichozipa fursa halmashauri kujitathmini na kuwa na mikakati thabiti, wakiwa kama Maafisa Masuhuli na wasimamizi wa makusanyo ya mapato ya serikali.
"Tunaishukuru TAKUKURU kwa kikao kazi hiki, kwa kuwa kimetuleta pamoja na kutujengea uelewa wa pamoja wa namna bora ya kuzuia mianya ya rushwa katika ukusanyaji wa mapato ya halmashauri zetu, niahidi kufanyia kazi maelekezo tuliyopewa, yakiwa na lengo la kuimarisha ukusanyaji wa mapato pamoja na matumizi sahihi ya mapato hayo kwa maendeleo ya wananchi wetu" Amefafanua Mkurugenzi Msumi
Kikao kazi hicho cha siku moja, kimewakutanisha wataalamu wa halmashauri, wakiwemo, Maafisa Mapato, Maafisa Biashara, Maafisa TEHAMA, Wakaguzi wa Ndani, Weka Hazina na Mawakala wa kukusanya mapato wakiongozwa na wakurugenzi wa halmashauri hizo hizo mbili.
ARUMERU
TUPO KAZINI✍✍✍
PICHA ZA MATUKIO YA KIKAO KAZI
Mkuu wa TAKUKURU wilaya ya Arumeru, Deo Mtui akizungumza wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha watalamu, wakusanya mapato na Mawakala wa mapato wa halmashauri zaArusha na Meru, kwenye ukumbi wa mikutano Chuo cha Ualimu Patandi.
Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi ( aliyesimama) akizungumza wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha watalamu, wakusanya mapato na Mawakala wa mapato wa halmashauri zaArusha na Meru, kwenye ukumbi wa mikutano Chuo cha Ualimu Patandi.
Afisa Mapato halmashauri ya Arusha, Ephata Swai, akizungumza wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha watalamu, wakusanya mapato na Mawakala wa mapato wa halmashauri zaArusha na Meru, kwenye ukumbi wa mikutano Chuo cha Ualimu Patandi.
Watalamu wa halmashauri za Arusha na Meru wakiwa kwenye kikao kazi na watalamu wa TAKUKURU, kilichofanyika kwenye ukumbi wa chuo cha Ualimu Patandi.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.