Na. Elinipa Lupembe.
Wanufaika wa mpango wa kunusuru Kaya Masikini, mradi unaotekelezwa na serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF, halmashauri ya Arusha wameendelea kuishukuru serikali kupitia mradi huo, wa kuwapatia ruzuku ya fedha kwa ajili ya kujikimu kimaisha.
Wakizungumza na mwandishi wetu, wakati wa zoezi la kupokea pesa, lililofanyika kwenye vijiji 45 vilivyo kwenye mpango halmashauri ya Arusha, wanufaika hao wamekiri licha ya kuwa fedha hizo ni kidogo lakini, zinawasaidia kupunguza makali ya maisha.
Suzana Mollel mkazi wa Sekei, amesema kuwa fedha hizo zimemuwezesha kujikwamua kimaisha ikiwemo, kutunza familia yake kwa kuwapatia mahitaji ya muhimu ikiwemo chakula na mavazi, sambamba na kununua mahitaji ya shule kwa watoto, jambo ambalo hapo awali lilikuwa ni kikwazo kutokana na uwezo duni aliokuwa nao.
"Ninafamilia ya watoto wanne wanaonitegemea, mume alinitelekeza muda mrefu, maisha yalikuwa magumu sana, zilipokuja hela za TASAF, zimenisaidika kupunguza makali ya maisha, nimeweza kufuga kuku na mbuzi, hali ya uchumi na maisha ya familia vimebadilika, ninaweza kujikimu, tofauti na hapo awali" amesema Suzana.
Naye Mwenyejiti wa kijiji cha Sekei, Miriam Lomayani, ameweka wazi kuwa, mradi huo wa TASAF wa kusaidia kaya masikini, umeziwezesha kaya nyingi kujikwamua kimaisha, kutokana na ukweli kwamba kabla ya mpango huo wa TASAF, kuna baadhi ya kaya zilikuwa na hali mbaya kiuchumi.
"Kwenye kijiji changu zipo kaya zimefanya mabadiliko kupitia pesa hizo, licha ya kwamba ni kidogo, wapo wanakaya waliotumia fedha hizo, kuwekeza kwenye miradi ya ufugaji kuku na mbuzi kilimo cha mbogamboga na biashara ndogondogo, jambo lililobadilisha hali zao za kimaisha za kaya hizo" amethibitisha Mwenyekiti huyo
Awali jumla ya shilingi milioni 239.3, zimetolewa ikiwa ni ruzuku ya miezi minne, baada ya kukamilika zoezi la uhakiki wa kaya zilizo kwenye mpango, na jumla ya kaya 6,811 zimepokea ruzuku hiyo.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.