Na. Elnipa Lupembe.
Serikali ya awamu ya tano, imeendelea kuweka mipango thabiti ya kumlinda mtoto wa kike kwa kuweka mazingira rafiki ya shuleni, ili kumuwezesha kusoma bila kubughudhiwa na changamoto za kijamii ikiwemo mimba na ndoa za utotoni, zinazomkabili mtoto wa kike katika kipindi cha masomo,lengo likiwa ni kupandisha kiwango cha taaluma na kuongeza ufaulu kwa wasichana.
Juhudi hizo zimefanywa na Serikali kupitia, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 75 za kujenga bweni la wasichana shule ya Sekondari Einoti kata ya Kisongo, halmashauri ya Arusha.
Akizungumza na mwandishi wetu, Mkuu wa shule ya sekondari Einoti, Mwalimu Justine Swai, ameeleza kuwa, licha ya kuwa uwepo wa bweni la wasichana shuleni hapo kupandisha kiwango cha taaluma na ufaulu kwa wanafunzi wasichana, utasaidia pia kuwaepusha watoto wa kike na changamoto za kijamii, zinazowakabili kutokana na mila na desturi za jamii za wafugaji, ikiwemo mimba na ndoa za utotoni pindi wanaporudi nyumbani kila siku.
"Katika jamii za wafugaji, elimu kwa mtoto wa kike sio kipaumbele, zaidi huandaliwa kwa ajili ya kuolewa, na mara nyingi hukosa muda wa kujisomea awapo nyumbani, kutokana na kupangiwa kazi za kufanya kila siku arudipo nyumbani, tofauti na mtoto wa kiume jambo ambalo linawarudisha nyuma kitaaluma na kushindwa kufanya vizuri kimasomo sawa na watoto wa kiume" ameleza Mkuu huyo wa shule.
Hata hivyo mwalimu Swai, amefafanua kuwa, kutokana na changamoto za mimba na ndoa za utotoni, shule iliamua kuanzisha madarasa mawili kutumika kama hosteli za wasichana, wenye changamoto za kijamii zinazofanywa na jamii za wafugaji,jaribio ambalo lilileta mafanikio kitaaluma na kijamii kwa wasichana shuleni hapo.
Aidha, Mkuu huyo wa shule, ameishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kujenga bweni la wasichana shuleni hapo, kwa kuwapunguzia kutembea umbali mrefu kutoka nyumbani, jambo litakalomfanya mwanafunzi kupata muda mrefu wa kujisomea na kujiepusha na mazingira hatarishi.
Afisa Elimu sekondari halmashauri ya Arusha, Menard Lupenza amesema kuwa, ujenzi wa bweni hilo la wasichana, unategemea kuwa na matokeo mazuri kitaaluma kwa wanafunzi hao, kutokana na kuishi katika mazingira bora jambo ambalo litarahisiha tendo la kujifunza kwa wanafunzi hao.
Ameongeza kuwa, lengo la serikali, ni kuweka mazingira bora ya kujifunzia kwa watoto wa kike, na kuwaepusha na changamoto za kijamii zinazowakabili kwa kuwawezesha kusoma kwa bidii bila kubughudhiwa, na kuwataka wasichana kutumia fursa hiyo muhimu kipindi chote wawapo shuleni.
Hata hivyo, Afisa Elimu huyo amefafanua kuwa, kiasi hicho cha fedha, kimejenga bweni moja lenye vyumba 22, ofisi ya matroni, vyoo na mabafu na sehemu ya kufulia, bweni ambalo litakalolaza wasichana 80, na linategemea kukamilika mapema mwezi Septemba.
Shule ya sekondari Einoti ina jumla ya wanafunzi 763, wavulana 276 na wasichana 485 na inafanya vizuri kitaaluma kwa matokeo ya kidato cha nne mwaka 2018 ilishika nafasi ya pili ngazi ya halmashauri ya Arusha.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.