Zoezo la ujenzi wa miundombinu ya kituo cha Afya Manyire kata ya Mlangarini, limeanza kwa kasi kubwa mara baada ya halmashauri ya Arusha, kupata fedha kutoka serikali ya Japani kupitia Ubalozi wa Japani nchini Tanzania.
Ubalozi huo wa Japani umetoa fedha kiasi cha shilingi milioni 191.9, kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa jengo hilo la kituo cha afya Manyire, mkataba uliosainiwa na pande zote mbili mwezi Machi,2018.
Afisa Mipango, halmashauri ya Arusha Anastazia Tutuba, amefafanua kuwa fedha hizo zitatumika kumalizia ujenzi pamoja na kununua samani.
"Katika milioni 191.9,kiasi cha shilingi milioni 143.9 kitatumika katika umaliziaji wa jengo hilo na shilingi milioni 48 zitatumika kununua samani za ndani ikiwemo vitanda vya wodi zote na chumba cha upasuaji" amethibitisha Afisa Mipango. Ameongeza kuwa, kituo hicho cha Afya kitaanza kutoa huduma, mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu ya jengo hilo.
Mhandisi wa Ujenzi halmashauri ya Arusha, Mhandisi Bibie Manzi, amesema kuwa kwa upande wa ujenzi, fedha hizo zitatumika kuweka sakafu kwenye kuta za jengo lote pamoja na sakafu ya chini, kuweka malumalu kwenye sakafu, dari, milango na madirisha pamoja na miundo mbinu yote ya maji na umeme mpaka kukamilika kwa jengo hilo.
Aidha Mhandisi Manzi amesema kuwa jengo hilo linategemea kukamilika mwanzoni mwa mwezi Septemba mwaka huu wa 2018.
Naye mganga mlezi wa kituo cha Afya Manyire, Dkt. Jafet Champanda, amesema kuwa, mara baada ya kukamilika kituo hicho, kinategemea kuhudumia zaidi ya watu elfu 6 na kaya 1200 zenye wastani wa watu watano kwa kila kaya wa kata ya Mlangarini na kijiji cha cha Marurani kata ya Nduruma.
Aidha Champanda ameongeza kuwa, kituo hicho cha afya kinategemea kutoa huduma zote za wagonjwa wa nje 'OPD' na kulaza jumla na kuongeza kuwa, kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kulaza jumla ya wagonjwa 56 kwa wakati mmoja.
Awali umaliziaji wa kituo hicho cha Afya, unakwenda sambamba na mkakati wa serikali ya awamu ya tano,wa kuhakikisha kila kata inakuwa na kituo cha afya chenye sifa ya nyota tano, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma zote muhimu za afya ndani ya kata zao pamoja na kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.