Na. Elinipa Lupembe.
Timu ya watalamu wasimamizi wa mradi wa maji wa vijiji vitano, maarufu kama mradi wa maji wa WaterAid, imetembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya mradi huo ulioanza kutekelezwa mapema mwezi Januari, 2019.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi, wakati wakati wa ziara hiyo, Mhandisi Mkazi wa shirika la WaterAid Tanzania, Mhandisi Jailos Chilewa amesema kuwa mpaka sasa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 35, ikijumuisha ujenzi wa matanki ya kuhifadhia maji, nyumba za kusimikia mitambo ya kutibu maji, nyumba za kuhifadhia pumpu, usambazaji wa mabomba, ujenzi wa vituo vya kuchotea maji (DPs) pamoja na ujenzi wa chanzo cha maji Emurtoto.
Mhandishi Chilewa amefafanua kuwa, mradi huo umegawanywa kwenye kandarasi nne, kutokana na ukubwa wa mradi na kuainisha kuwa, Lot I ya mradi inatekelezwa na kampuni ya STC Construction Company Ltd, ambao wamefikia asilimia 20%, Lot II unajengwa na kampuni za Advance Company Ltd & Meero Contractors Ltd na umefikia asilimia 59%, Lot III unatekelezwa na Kampuni ya ASSES Ltd ambao wamefikia asilimia 78%, huku Lot IV ukitekelezwa na Kampuni ya Daviss and Shirtliff waliofikia asilimia 21%
Ameongeza kuwa licha ya utekelezaji wa ujenzi kuendelea vizuri na kufikia asilimia hizo, bado wakandarasi hao wako nyuma ya muda, kulingana na muda wa kwenye mikataba yao, hali iliyosababishwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kimazingira kwa baadhi ya maeneo.
Hata hivyo timu hiyo imewaagiza timu ya watalamu wasimamizi wa ujenzi, kuongezeka kwa kasi ya usimamizi na kuhakikisha wakandarasi hao, wanafanya kazi usiku na mchana pamoja na kuwawezesha kukabiliana na aina yoyote ya changamoto zinazojitokeza wakati wa ujenzi wa mradi huo.
Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arudha Dkt. Wilson Mahera amesema kuwa, wameweka mkakati wa kuhakikisha watalamu hao, wanawasimamia kwa karibu wakandarasi hao na kushirikiana nao kama timu ili kutatua changamoto zitakazojitokeza wakati wa ujenzi kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata maji kama Serikali ilivyokusudia.
Naye mkurugenzi wa shirika la WaterAid Tanzania, Dkt. Ibrahim Kabole amewasisitiza wakandarasi wanaojenga mradi huo kuwa, licha ya changamoto zote zinazojitokeza wakati wa ujenzi wa mradi huo, lengo kubwa la shirika hilo na wafadhili wa mradi huo, ni wananchi wa vijiji lengwa, kupata maji safi na salama kabla ya mwaka huu wa fedha kukamilika.
" Pambaneni na changamoto zote ' but at the end of the day wananchi wanatakiwa kupata maji safi na salama, hilo ndio lengo la wafadhili DFID na lengo letu kama wasimamizi wa mradi" amesisitiza Dkt. Kabole.
Mradi wa maji wa vijiji vitano, unaotekelezwa na shirika la WaterAid Tanzania, kwa ufadhili wa Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya nchini Uingereza 'DFID' kwa gharama ya shilingi bilioni 8.4, umelenga kuhudumia takribani watu 50,000 wa vijiji vya Lengijave, Olkokola na vitongoji vya Seuri, Ekenywa na Ngaramtoni, na unategemea kukamilka mwishoni mwa mwaka huu wa fedha, ifikapo mwezi Juni 2019.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.