Viongozi wa ngazi za vijiji,vitongoji na kata, halmashauri ya Arusha wametakiwa kutoa elimu kwa wananchi wanaowaongoza ili waweze kuithamini miradi ya maendeleo, inayotekelezwa katika maeneo yao.
Rai hiyo imetolewa na Mhandisi wa Maji mkoa wa Arusha, Mhandisi Joseph Makaidi, wakati akiwasilisha mrejesho wa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa maji wa vijiji vitano, unaofadhiliwa na Idara ya Maendeleo ya nchini Uingereza 'DFID' kwa gharama ya shilingi bilioni 4.5.
Mhandisi Makaidi amesema kuwa, viongozi wa jamii wanao wajibu wa kuwaelimisha wananchi wao, kutambua miradi hiyo kuwa ni mali yao pamoja na kuwashirikisha katika hatua mbalimbali za maamuzi kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo, inayotekelezwa kwenye maeneo yao.
" Kama wananchu hawashirikishwi kikamilifu kuanzia mradibunaanza na hatua mbalimbali za mradi husababisha wananchi kuihujumu miradi wakati wa utekelezaji na pia katika uendeshaji wa miradi, miradi mingi imekwama kutokana na wananchi kutokuwa na taarifa sahihi za miradi hiyo" amesema Mhandisi huyo. Ameongeza kuwa, miradi mingi itakuwa endelevu, endapo wananchi wataifahamu kuanzia mwanzo, hatua zote za utekelezaji mpaka kukamilika kwake. Hali hii itawapa nafasi wananchi kuisimamia miradi hiyo kwa dhati, huku wakifahamu na kutambua kuwa miradi hiyo ni mali yao.
Naye diwani wa kata ya Olkokola,na aliyekuwa mwenyekiti wa kikao kazi hicho, mheshimiwa Kalanga Laizer amesema kwamba,kutokana na ushirikishwaji wa wananchi katika hatua zote za mradi wa maji wa vijiji vitano, jamii imeridhika hasa katika ushirikishwaji ulivyoanza na vikao vya wananchi kujengewa uwezo na kuwa na uelewa wa pamoja juu ya mradi huo.
Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Dkt. Wilson Mahera, ameikumbusha jamii kutambua umuhimu wa utunzaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao, sambamba na kukubali kukabiliana na changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi na wakati wa uendeshaji wa mradi pia.
Hata hivyo Mkurugenzi Mahera, amewahakikishia viongozi na wananchi wa halmashauri ya Arusha usimamizi thabiti wa utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya halmashauri licha ya kuwepo changamoto nyingi wakati wa utekelezaji wa miradi.
Aidha Dkt. Mahera ameupa kipaumbele mradi huu mpya wa maji wa vijiji vitano, ambao kimsingi utasaidia kupunguza adha ya maji kwa zaidi ya wananchi elfu hamsini wa kata nne na vijiji viwili na vitongoji vitatu, mradi utakaokwenda na teknolojia mpya kulipia maji kabla ya kutumia.
Kikao kazi hicho, kimewakutanisha wadau wote wanaoshiriki katika utekelezaji wa mradi wa maji wa vijiji vitano uliojumuisha, wadau wa kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi cha Nelson Mandela, Tumaini Jipya-New Hope, shirika la WaterAid na eWater kwa kujuisha watalamu wa ngazi ya halmashauri, vijiji na kata, viongozi wawakilishi wa jamii wa kata za nne za eneo la mradi za Lemanyata, Olkokola, Olmotonyi na Olturumet.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.