Na. Elinipa Lupembe.
Wananchi wa kijiji cha Engalaoni kata ya Mwandet, halmashauri ya Arusha, wameamua kuunganisha nguvu pamoja na kuanza ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Engalaoni, baada ya kukerwa na adha wanayoipata watoto wao ya kujazana kwnye vyumba vya madarasa wakati wa masomo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, alipotembelea shuleni hapo, Mwenyekiti wa Kamati ya shule, Christopher Laiser, amesema kuwa Wananchi hao wa kijiji cha Engalaoni, wameamua kuanza ujenzi wa vyumba 3 vya madarasa lwa lengo la kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani kutokana na ongezeko la idadi kubwa ya wanafunzi linalotokana na Elimu bila Malipo.
Amefafanua kuwa hamasa ya ujenzi huo wa vyumba vya madarasa, umekuja baada ya serikali kutoa elimu bila malipo, hali ambayo imeondoa vikwazo kwa wazazi wengi na kulazimika kupeleka watoto shule pamoja na wananchi kuanza kupata mwamko wa kuwapeleka watoto wao shule.
"Ujenzi huo wa vyumba 3 vya madarasa, umeanza mapema mwezi wa Juni na umefikia hatua ya kupaua sasa, ujenzi utagharimu shilingi milioni 37 kila darasa likigharimu shilingi milioni 13 kwa kila darasa, mpaka kukamilika kwake" amesema Mwenyekiti huyo.
Ili kukamilisha ujenzi huo, wananchi wa Engalaoni wanachangia kiasi cha shilingi elfu 42 kwa kila mkuu wa kaya ambaye ni mwanaume pamoja na nguvu kazi kwa wananchi wote, na tayari vifaa vya kukamilisha ujenzi huo vimekwisha nunuliwa viko stoo, tayari kwa ukamilshaji wa jengo hilo kabla ya mwezi Oktoba.
Naye Mwalimu mkuu shule ya msingi Engalaoni, mwalimu Ester Kimaro, licha ya kuwashukuru na kuawapongeza wananchi wa kijiji hicha, ameeleza kuwa, ujenzi huo wa vyumba hivyo vya madarasa, utapunguza msongamano wa wanafunzi darasani kwa kiasi, kutokana na shule hiyo kuwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa.
" Shule ina hii ina jumla ya wanafunzi 1,283 ikiwa na vyumba 9 vya madarasa, idadi inayolazimu zaidi ya wanafunzi 100 kukaa kwenye chumba kimoja cha darasa, hali iliyosababaishwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaoandikishwa shuleni hapo, tangu serikali kutekeleza sera ya elimu bila". Amesema mwalimu Ester.
Hata hivyo mipango ya wananchi wa Engalaoni kabla ya mwaka huu kumalizika ni kujenga vyumba vingine viwili vya madarasa pamoja na nyumba za walimu, kutokana na walimu wengi kukosa mahali pa kuishi katika maeneo hayo yasiyo na nyumba za kupangisha.
Halmashauri ya Arusha inatoa kongole kwa wananachi wa Engalaoni kwa mchango wao mkubwa kwenye sekta ya Elimu, zaidi inawahamasisha wadau wa elimu kutoka mashirika, taasisi na makampuni binafisi, kujitokeza kuchangia na kuwaunga mkono wananchi wa engalaoni kwa ajili ya mtoto wa kitanzania.
PICHA ZA VYUMBA VYA MADARASA S/M ENGALAONI
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.