Na. Elinipa Lupembe
Wafugaji Halmashauri ya Arusha, wametakiwa kutumia majosho, kuogesha mifugo yao, ili kuwa na mifugo yenye afya bora, mifugo ambayo itakuwa na tija na kuwaongezea kipato sambamba na kupandisha hali ya uchumi wa familia na Taifa.
Rai hiyo imetolewa na mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi, wakati akizindua josho la Kanda C, lililofanyiwa ukarabati na wafugaji wa katika kijiji cha Lemanda kata ya Oldonyosambu, mara baada ya serikali kuanzisha mkakati wa kutoa dawa za kuogeshea mifugo kwa wafugaji.
Mkurugenzi Msumi, licha ya kuwapongeza wafugaji hao kwa kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita, na kuona umuhimu wa kufanya ukarabati wa josho hilo, ili kuikinga na vifo vinavyotokana na magonjwa yanayoenezwa na wadudu aina ya kupe na ndorobo, magonjwa ambayo yanauwa mifigo kwa zaidi ya asilimia 70 mpaka 100, amewataka wafugaji hao kufanya ufugaji wenye tija kwa kuogesha mifugo pamoja na kuipatia chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali.
"Niwatake wafugaji, kuacha kufuga kwa mazoea, fugeni mifugo michache yenye tija, fugeni kwa kiasi, mifugo ambayo mtaweza kuihudumia kwa kuipa chanjo na kuiogesha, ili mifugo hiyo iweze kuwaingizia kipato, tumieni josho hili, kuogesha mifugo yenu, kama watalamu wa mifugo wanavyowaelekeza, hakikisheni mnakuwa na ng'ombe bora, mtakawapeleka sokoni na kuuza kwa bei nzuri" amesisitiza Mkurugenzi Msumi.
Hata hivyo wafugaji hao wa kijiji cha Lemanda, wameishukuru serikali kupitia Wizara ya Mifugo, kwa kuwapatia ruzuku ya dawa ya kuogeshea mifugo, dawa ambayo imewasukuma kukarabati josho hilo, josho ambalo liliacha kutumika zaidi ya miaka 20, kutokana na kushindwa kujiendesha.
Mwenyekiti wa kamati ya kusimamia uendeshaji wa josho la Kanda C, Peter Leskari amesema kuwa, kuzinduliwa kwa josho hilo, kutarudisha matumaini kwa wafugaji, matumaini ambayo yalipotea kwa muda mrefu, ambapo wafugaji walipoteza mifugo yao kutokana na vifo vilivyotokana na magonjwa yanayotokana na kupe na ndorobo na kuahidi kusimamia uendeshaji wa josho hilo ili liwanufaishe wafugaji wote wa eneo hilo.
"Josho hili linatupa uhakika wafugaji wa kuwa na mifugo yenye afya bora, wafugaji wengi walishindwa kumudu gharama kubwa za kuogesha mifugo nyumbani, ng'ombe wengi walikufa na kuzorotesha uchumi wa wafugaji, kupitia josho hili, tumerudisha matumaini kwa wafugaji sasa" ameweka wazi Mwenyekiti huyo wa kamati ya Josho.
Naye Afisa Mifugo halmashauri ya Arusha, Omary Sembe, amefafanua kuwa, serikali kupitia wizara ya mifugo, inatekeleza mkakati wa kuboresha sekta ya mifugo na wafugaji, kwa kutoa dawa za kuogeshea mifugo bure, ili kuzuia vifo vinavyotokana na magonjwa ya kupe na ndorobo, magonjwa ambayo yanaua mifugo kwa zaidi ya asilimia 90.
"Dawa hii ya kuogeshea mifugo, inauwezo wa kuikinga mifugo kwa zaidi ya asilimia 70 ya magonjwa yanayotokana na kupe na ndorobo, ikiwemo magonjwa ya ndigana kali, ndigana baridi, moyo kujaa maj, .....hivyo kuogesha mifugo, kutaondoa vifo vya mifugo visivyo vya lazima" amefafanua Afisa Mifugo.
Awali josho hilo la Kanda C, limekarabatiwa na wafugaji wa kijiji cha Lemanda kwa kushirikiana na halmashauri, kwa gharama ya shilingi milioni 2.8, baada ya srikali kutoa lita elfu 15 za dawa ya kuogeshea mifugo, josho linategema kuogesha jumla mifugo elfu 90, ng'ombe elfu 15, kondooo elfu 42 na mbuzi elfu 33.
Arusha DC
Kazi Inaendelea✍✍✍
Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri yaArusha, Seleman Msumi, akichanganya dawa ya kuogeshea mifugo, tayari kwa uzinduzi wa josho la Kanda C, kijiji cha Lemamnda kata ya Oldonyosambu.
Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri yaArusha, Seleman Msumi, akimimina dawa ya kuogeshea mifugo, kwenye josho la Kanda C, kijiji cha Lemamnda kata ya Oldonyosambu, ikiwa ni ishara ya kuzindua josho hilo.
Zoezi la uogeshaji mifugo, limeanza rasmi, mara baada ya uzinduzi wa josho la Kanda C, kijiji cha Lemanda.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.