Na. Elinipa Lupembe
Wajumbe wa Kamati ya kupinga Ukatili dhidi ya Watoto na Wanawake halmsahauri ya Arusha wameiomba halmashauri hiyo, kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kuwatunzia watoto waliofanyiwa vitendo vya ukatili, maarufu kama Nyumba Salama.
Wajumbe hao wamefikia maamuzi ya kufikisha ombi hilo kwa Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha, baada ya kukutana na changamoto ya mahali pa kuwatunza watoto walipota madhila ya kufanyiwa vitendo vya ukatili, azimio lililofikiwa wakati wa kikao maalum cha kamati hiyo kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Kijiji cha Watoto SOS - Ngaramtoni.
Wajumbe hao wamebainisha changamoto hiyo ya muda mrefu, ya halmashauri hiyo kukosa kituo cha kudumu cha Nyumba Salama, kwa ajili ya kuwahifadhi na kuwatunza watoto wenye mgogoro wa kisheria, wakati kesi zao zinaaendelea kusikilizwa, imesababisha baadhi ya kesi kupoteza uhalisia na ushahidi na hatimaye watuhumiwa kuachiwa huru.
"Halmashauri ya Arusha haina kituo maalum kwa ajili ya kuhifadhi watoto, waliofanyiwa vitendo vya ukatili, tunalazimika kuwaapeleka kwenye kituo kilichopo Jiji la Arusha, jambo ambalo kituo kile kinaelemewa na idadi kubwa ya watoto, hivyo ni vema halmashauri ya Arusha ikawa na Nyumba salama yake" amefafanua Afisa Jinsia Rovil Nguyaine
Hata hivyo wajumbe hao wamebainisa umuhimu wa Nyumba Salama ni kutokana na ukweli kwamba, tafiti zinaonesha watoto wengi hufanyiwa vitendo vya ukatili na watu walio ndani ya familia ndani na jamii zao, jambo ambalo linaonekana endapo mtoto atafanyiwa ukatili na tukio hilo kupelekwa kwenye vyombo vya sheria, kuendelea kukaa kwenye familia au jamii iliyomtendea ukatili huo, ni rahisi mtoto huyo kushawishika na kupoteza ushahidi wa kesi husika.
Mwaansheri wa Halmashuri ya Arusha, Eliasifiwe Kileo, amebainisha kuwa, ni hatari sana mtoto, aliyefanyiwa ukatili kuendelea kuishi kwenye familia au jamii iliyomfanyia ukatili, jambo ambalo huzuia kupatikana kwa ushahidi halisi wa kesi hiyo sambamba na kupoteza haki ya mtoto husika.
"Mtoto aliyefanyiwa vitendo vya ukatili, akiendelea kukaa kwenye familia au jamii, iliyomfanyia ukatili huo, mara nyingi ushahidi wa kesi hizo huharibiwa kwa mtoto kurubuniwa au kushawishiwa na familia, ili kuharibu ushahidi, jambo ambalo humkosesha mtoto, haki yake ya msingi kisheria" amesisiituza Mwanasheri huyo
Naye Kaimu Mkurugenzi halmashauri ya Arusha na Afisa Mifugo Wilaya Omary Sembe, amekiri kutambua umuhimu wa kituo hicho na kuahidi kufikisha jambo hilo kwenye menejimenti ili litafutiwe ufumbuzi wa haraka, kutokana na umuhimu wake, na hatimaye halmashauri ya Arusha kuwa Nyumba Salama, kama ilivyo takwa na agizo la Serikali kwa maslahi ya watoto na Taifa kwa ujumla.
Hata hivyo baadhi ya Wadau wa masuala ya watoto na wanawake, ambao ni wajumbe wa Kamati hiyo, wameweka wazi kuwa, kutokana na umuhimu wa kituo hicho, endapo halmashauri itatoa eneo kwa ajili ya ujenzi, watakuwa tayari kushiriki ujenzi wa Nyumba hiyo salama.
.ARUSHA DC 4
KaziInaendelea✍✍✍
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.