Na Elinipa Lupembe
Walimu 1,442 wa shule za msingi na sekondari halmashauri ya Arusha wamekabidhiwa vishikwambi, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya serikali yaliyotolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa
Akikabidhi vishikwambi hivyo, Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Mhandisi Richard Ruyango amewataka walimu kutumia nyenzo hizo muhimu za kidijitali kwa lengo lililokusudiwa ikiwa ni pamoja na kupandisha kiwango cha taaluma shuleni.
"Seikali imeona umumimu wa walimu kupatiwa vitendea kazi vya kidigitali ili kurahisisha tendo la kufundisha na kujifunzia, walimu mnalo jukumu la kuvitumia kulingana na maelekezo pamoja na kuvitunza ili kufikia lengo la serikali". Amesisitiza Mhandisi Ruyango
Naye Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi amesema kuwa vishikwambi hivyo vinapaswa kutumiwa kwa mujibu wa miongozo ya Serikali ni mali ya Umma na vitasimamiwa kwa mujibu wa sheria ya manunuzi ya Umma na kanuni zake.
Ameongeza kuwa mwalimu anatakuwa kutumia vishikwambi hivyo kwa ajili ya kupata matini ya masomo, vitabu rejea pamoja na picha za video zinazohusu masomo na si vinginevyo.
Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi Mwl. Salvatory Alute licha ya kuishukuru serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na mama Samia Suluhu, ameahidi kusimamia matumizi na utunzaji wa vishikwambi hivyo, na kuhakikisha vinatumika kupandisha taaluma shuleni na kufikia lengo la serikali.
"Tunaamini matumizi ya teknolojia rahisi shuleni, yanakwenda kufanya mapinduzi ya kitaaluma kwa kumuwezesha mwalimu kupata maarifa na ujuzi ikiwemo matini ya masomo, mbinu za kufundishia na kujifunzia kuendana na mabadiliko ya Sayansi na teknolojia". Amebainisha Afisa Elimu Mkuu Mwl. Alute
Hata hivyo walimu hawakusita kumshukuru mhe. Rais Samia Suluhu, kwa kuona umuhimu wa walimu kuwa na kitendea kinachowatoa kwenye analojia na kuwapeleka kwenye dijitali.
Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Lesiraa, Mwl. Dora Ngobei amethibitisha kuwa vishikwambi hivyo ni nyenzo muhimu na rahisi itakayomuwezesha mwalimu, kupata na kuhifadhi matini ya masomo, pamoja na vitabu rejea vitakavyomjenga kuwa na maarifa mapya kila wakati.
"Hiki ni kitendea kazi muhimu kwa mwalimu, licha ya kupunguza gharama ya matumizi ya karatasi, kitasaidia pia ujazaji wa taarifa kwenye mifumo, ambapo awali ilikuwa ngumu kwa shule ambazo hazikuwa na kompyuta". Amesema Mkuu wa shule sekondari Likamba Mw. Richard Mugyabuso
Awali Mkuu huyo wa wilaya amekabidhi vishkwambi hivyo kwa wakuu wa shule za sekondari, walimu wakuu wa shule za msingi pamoja na maafisa elimu wa kata zote kwa niaba ya walimu wote, zoezi lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano halmashauri hiyo.
ARUSHA DC
KaziInaendelea✍✍
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.