Wananchi halmashauri ya Arusha wameshiriki maadhimisho ya Siku ya Afya ya Mazingira Duniani, kwa kufanya usafi maalum kwenye maeneo yao, huku kilele cha maadhimisho hayo kikifanyika kwenye kata ya Olmotonyi.
Wananchi hao wamefanya usafi kwenye maeneo yanayowazunguka pamoja na maeneo ya wazi huku wakiiomba Serikali kutilia mkazo suala la Usafi ili kudumisha afya za wananchi kwa Maafisa Afya kutembelea wananchi kila wakati na kutoa elimu juu ya umuhimu wa kufanya usafi kwenye maeneo yao.
Akizungumza mmoja wa wananchi hao wakati wa zoezi hilo la usafi, Linda Hagai ambaye ni mhudumu wa mgahawa, amesema kuwa siku hiyo ni muhimu sana kwaajili ya kuhamasisha wananchi kujiwekea tamaduni za kudumisha usafi kwenye maeneo yanayowazunguka ndani na nje.
"Tunaiomba serikali iendelee kututembea na kuhamasisha suala la usafi ili kila mwanachi awe na uelewa juu ya suala hili na sio tu kufanya hivyo wakati wa maadhimisho ya siku hii". Amesisitiza Linda.
Adinan Msangi aliyeshika kandarasi ya kukusanya taka ngumu eneo la Olmotony, amesema kuwa,wananchi wameadhimisha siku hiyo kwa kufanya usafi wa maeneo ma kuongeza kuwa kila mara wamekuwa wakiwahasisha wananchi kusafisha mazingira yao pamoja na kuhakikisha wanahifadhi taka vizuri mpaka hapo zitakapochukuliwa na magari ya taka.
Hata hivyo Afisa wa Afya halmashauri ya Arusha, Issa Msumari ametoa rai kwa wananchi wote wa halmashauri hiyo kuhakikisha wanafanya usafi wa mazingira kila wakati pamoja na kuweka misingi thabiti ya matumizi sahihi ya vyoo, unawaji mikono baada ya kutoka chooni, uhifadhi na utupaji wa taka ulisahihi ili kuboresha afya ya Jamii na kuepukana na magonjwa ya mlipuko.
"Kupitia siku hii muhimu, tunawahamasisha wananchi wote ndani ya halmashauri yetu kuhakikisha kwamba wanazingatia vigezo na misingi yote ya afya ili tuweze kuboresha afya ya jamii na kuepukana na magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu". Amesema Afisa Afya huyo.
Ameongeza kuwa halmashauri ya Arusha kwa kushirikiana na wadau wa afya, jeshi la polisi na wanachi wamefanya usafi wa kuzunguka maeneo ya kata ya Olmotony na vitongoji vyake huku kila mmoja akitakiwa kuzingatia kanuni mbalimbali za afya ili kujinga na magonjwa ya mlipuko yatokanayo na uchafu
Siku ya Afya ya Mazingira Duniani imeasisiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa lengo la kutoa fursa ya kuchukua hatua na kuhamasisha jamii kuhusu masuala yanayohusiana na afya ya mazingira huku masuala ya uchafuzi wa hewa, maji na udongo, matumizi ya kemikali hatari, uchafuzi wa mazingira vijijini na mijini, kuhifadhi bioanuwai, mabadiliko ya tabianchi, usafi wa mazingira na utawala bora wa mazingira yakitiliwa mkazo na huadhimishwa mwezi Septemba kila mmwaka
ARUSHA DC NI YETU, TUSHIRIKIANE KUIJENGA
#KaziIendelee✍
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.