Wananchi halmashauri ya Arusha, wametakiwa kuwa na tabia chanya za afya, za kuzingatia usafi wa mazingira na usafi wao binafsi, kwa kuwa na vyoo bora na tabia inayoendana na matumizi sahihi ya vyoo na unawaji mikono kwa sabuni katika nyakati tano muhimu.
Rai hiyo imetolewa na Afisa Tarafa ya Muklat Hudhaifa Rashid, kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Arumeru, wakati wa Tamasha la Uzinduzi wa kuhamasisha mbinu shirikishi ya tabia chanya za Afya, tamasha lililofanyika kwenye viwanja vya Stendi ya Daladala Ngaramtoni, mwishoni mwa juma iliyopita
Afisa Tarafa huyo amesema, lengo la Serikali ni kuwa na Taifa lenye watu wenye afya bora, afya zinazolindwa na watu wanaojali afya zao wenyewe, kwa kuwa na tabia chanya za afya, ili kuondokana na magonjwa yanayoweza kuzuilika kwa gharama ndogo, gharama ya kubadili tabia.
Amesema kuwa asilimia 70 ya magonjwa yanayowasumbua watanzania, yanatokana na kutokufuata tabia chanya za afya, ambazo husababisha, uchafu wa mazingira na uchafu binafsi, jambo ambalo watu wakibadili tabia magonjwa hayo yanaweza kutoweka, na kuendelea kupambana na masuala mengine ya maendeleo na si suala la usafi.
Amezitaja tabia chanya za afya ni pamoja na matumizi sahihi ya vyoo, kunawa mikono katika nyakati muhimu,usafi wa vyakula na matumizi ya maji safi na salama ya kunywa, na kufafanua kuwa, nyakati tano muhimu za kunawa mikono ni pamoja na baada yakutoka chooni, kabla ya kula, kabla ya kuandaa chakula,kabla ya kumnyonyesha mtoto na baada ya kumsafisha mtoto aliejisaidia (kunya)
Rashid amesisitiza kuwa, kama Serikali inatumia nguvu kubwa, kuwekeza kwenye maendeleo ya kiuchumi ni vema wananchi wakabadili tabia ili kuepuko vifo vinavyoweza kuzuilika, na baadaye kuweza kufaidi matunda ya maendeleo yanayofanywa na serikali yao ya sasa ya awamu ya tano.
"Serikali ya awamu ya tano, inayoongozwa na Dr. John Pombe Magufuli, inaweka juhudi kubwa kuboresha huduma za jamii, hivyo ni wajibu wetu sasa kuhakikisha tunafaidi matunda hayo, kwa kuwa na taifa kenye watu wenye afya bora" amesema Rashid.
Naye Naivasha Lukas, mkazi wa Ngaramtoni amesema kuwa, kwa sasa wananchi wengi wamefahamu umuhimu wa kuwa na choo bora pamoja na matumizi yake, tofauti na hapo awali, kutokana na tamaduni zao, hakukuwa na umuhimu na kuthibitisha kuwa, kampeni ya Nyumba ni Choo, imewafumbua macho na zaidi imewesha kaya nyingi kuwa na vyoo kwa sasa.
Naye Afisa Afya, halmashauri ya Arusha, Issa Msumari amesema kuwa, halmashauri inatekeleza kampeni ya kitaifa ya Usafi wa Mazingira, kampeni iliyoleta matoke chanya, mpaka sasa asilimia 73 ya kaya ndani ya halmashauri hiyo zina vyoo.
Mpaka kufikia aslimia 73 ya kaya zenye vyoo bira, asilimia 24 kaya zenye vyoo vya asili na kufikisha asilimia 98 ya kaya zenye vyoo ndani ya halmashauri hiyo.
Hata hivyo, Afisa Afya huyo, ameweka wazi kuwa, kampeni ya kitaifa ya Usafi wa Mazingira, imewezesha halmashauri kufikisha asilimia 98 ya kaya kuwa na vyoo,kupitia mkakati wa kuunda kamati za ufuatiliaji katika ngazi za Vitongoji, na kuongeza kuwa mpaka kufikia mwaka 2020, kaya zenye vyoo vya asili zitakuwa na vyoo bora na kaya zisizo na vyoo kuwa na vyoo.
Tamasha hilo liliambatana burudani mbalimbali pamoja na utoaji wa zawadi kwa washindi watano wa usafi wa mazingira kati ya kata 27 za halmashauri ya Arusha, ambapo kata ya Oloirien iliibuka kidedea, na kufuatiwa na kata ya Ilikiding'a, kata ya Olmotonyi, kata ya Lemanyata na kata ya Moivo likiwa na kaulimbiu inayosema 'Usichukulie Poa, nyumba ni Choo'
Awali Tamasha hilo, limefanikishwa na halmashauri ya Arusha kwa kushirikiana na wadau wa shirika la WaterAid-Tanzania, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wz mradi wa maji wa vijiji vitano, uliofadhiliwa na DFID.
Afisa Tarafa ya Mukulat, Hudhaifa Rashid akizungumza kwenye Tamasha la mbinu maalumu za kuhamasisha tabia chanya za afya, kwenye viwanja vya Stendi ya Daladala Ngaramtoni.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.