Na Elinipa Lupembe
Wananchi wa kijiji cha Lemanda kata ya Oldongosambu wamemshukuru Mhe. Rais mama Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa mradi wa ujenzi wa shule mpya ya msingi kijijini kwao.
Wakizungumza mbele ya Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Mhe. Emmanuela Mtatifikolo Kaganda, kwenye eneo la mradi huo, wamesema kuwa uwepo wa shule kijijini hapo, utawapa fursa watoto wao kupata elimu na kutimiza ndoto zao, tofauti na hapo awali ambapo watoto wengi hawakusoma na wasichana kuolewa kwenye umri mdogo.
Wamesema kuwa kutokana na ukubwa wa kijiji na kata hiyo yenye shule mbili za msingi, watoto hulazimika kutembea umnali wa zaidi ya Km 18 mpaka 20 kwenda na kurudi shuleni, jambo ambalo lilikatisha tamaa watoto wengi na kuamua kuacha shule na wengi kutokufanya vizuri kwenye mitihani yao huku watoto wadogo wakiandikishwa shule kwa kuchelewa kwa kuhofia umbali huo.
Faraja Charles (27) Mama wa watoto watatu ametuma salamu za shukrani kwa mama Samia, kwa kuwajali kinamama wa Lemanda kwa kusogeza shule kijijini kwao, jambo ambalo lilikuwa ni ndoto, huku wakiamini watoto wao kupata elimu kama ilivyo watoto wengine wa kitanzania.
Kiongozi wa mila wa ukoo wa Lukumai, Laigwanani Saringe Naromosha, amesema kuwa wameona serikali inafanya kazi, walikuwa na njaa ikawaletea mahindi na muda mfupi akaleta pesa za kujenga shule.
"Sisi tulidhani serikali itapambana na njaa tuu, lakini punde si punde imeleta mradi wa shule, tunamshukuru sana mama Samia na tunamuombea kwa Mungu, aongoze vizuri kwa kuwajali wananchi wa hali ya chini" Amethibitisha Laigwanani huyo.
Diwani wa kata ya Oldonyosambu, Raymond Rairumbe, amemshukuru Mhe. Rais kupitia mradi huo wa fedha nyingi kijijini hapo, mradi ambao unakwenda kuwahudumia watoto wa familia za wafugaji ambao wengi walikosa fursa hiyo tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika
"Kiukweli tumeshuhudia serikali ya awamu ya sita ikifanya kazi, kata hii imepata zaidi ya 45% ya fedha zote za mradi wa BOOST zilizoletwa halmashauri ya Arusha, tumepata milioni 306 .9 kati ya milioni 682.5, kiasi ambacho ni kikubwa ukilinganisha na fedha zilizokwenda maeneo mengine, tunathibitisha mama yuko kazini, Nani kama mama" Ameweka wazi Mhe. Diwani huyo.
Shule mpya ya msingi, inajengwa kwa gahrama ya shilingi milioni 306.9 ikijumuisha ujenzi wa vyumba 2 vya madarasa ya awali, vyumba 7 vya madarasa ya msingi, matundu 16 ya vyoo pamoja na jengo la utawala.
Awali, jumla ya shilingi milioni 682.5 kutoka Serikali Kuu kupitia Mradi wa Kuboresha Upatikanaji wa Fursa sawa katika Ujifunzaji Bora kwa Elimu ya Awali na Msingi Tanzania Bara (BOOST), fedha zitakazotumika katika ujenzi wa miundombinu ya shule 6 za Awali na Msingi.
Ikumbukwe kuwa, miradi hiyo ya ujenzi wa miundombinu shule za msingi ni utekelezaji wa Ilani ya CCM, Sura ya tatu Ibara ya 79 kifungu (q)Kukarabati miundombinu ya kufundishia na kujifunzia na kifungu (C)Kuboresha uratibu na usimamiaji wa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu.
ARUSHA DC ni Yetu, Tushirikiane Kuijenga"
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.