Na. Elinipa Lupembe.
Wananchi wa kijiji cha Losinoni Juu kata ya Oldonyowas, halmashauri ya Arusha, wilaya ya Arumeru, wamepata utatuzi wa changamoto ya Vifo vya kinamama na watoto wakati wa kujifungua, vilivyosababishwa na ukosefu wa Zahanati katika kijiji hicho kwa miaka nenda rudi.
Changamoto hiyo imepata ufumbuzi wa kudumu, mara baada ya shirika la Friends of Tanzania - ARUSHA, kwa kupitia ufadhili wa wananchi wa nchini Ujerumani, kukamilisha ujenzi wa zahanati ya Losinoni Juu na kuikabidhi kwa Serikali ya Kijiji cha Losinoni Juu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi na kukabidhi Zahanati hiyo, Mratibu wa mradi shirika la Friends in Tanzania -ARUSHA, Harald Pfiffer, amesema kuwa, wananchi wa Ujerumani walitambua changamoto za huduma za afya, zilizokuwa zikiwakabili wananchi wa Losinoni Juu, na kuona umuhimu wa kuwajengea Zahanati hiyo ili kuokoa maisha ya wananchi wa eneo hilo.
Pfiffer ameongeza kuwa, licha ya yeye kuwa rafiki wa wananchi wa Losinoni Juu, kwa muda mrefu sasa, lakini ameridhishwa zaidi na uongozi wa Rais John Pombe Magufuli wa kuwahudumia wananchi hasa wa vijijini, maeneo ambayo kuna changamoto nyingi za kijamii na kuwataka wananchi hao kukitumia kituo hicho pamoja na kutunza jengo hilo.
Naye mgeni rasmi na mkuu wa wilaya ya Arumeru, Jerry Muro amelishukuru shirika hilo, kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano, na kuwaomba wadau hao kuendelea kusaidia ujenzi wa nyumba za watumishi ili huduma hiyo, iweze kutolewa kwa saa 24 na siku saba za wiki.
Aidha mkuu wa Wilaya huyo, amewataka wananchi wa kijiji hicho, kutumia Zahanati hiyo, na kuwasisitiza kina mama wajawazito kuhudhuria Kiliniki muda wote wa ujauzito, kuacha tabia ya kujifungulia nyumbani pamoja na kuwapeleka watoto wa umri wa chini ya miaka mitano kupata chanjo zote zinazostahili.
Ameongeza kuwa, lengo la serikali ya awamu ya tano, ni kupunguza na kutokomeza vifo vya mama na mtoto, kwa kusogeza huduma za afya kwa wananchi, kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na Zahanati, kata kuwa na kituo cha Afya pamoja na hospital za Wilaya na mikoa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya.
"Serikali ya awamu ya tano, inashirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi, kutokomeza vifo vya mama na mtoto, tunahakikisha kila huduma zinapatikana kuanzia ngazi ya kijiji kuwe na Zahanati, kila kata iwe na kituo cha afya, hospitali za wilaya na za mkoa" amesisitiza mkuu huyo wa wilaya.
Mheshimiwa Muro, amefafanua kuwa, serikali itahakikisha kuleta watumishi watakaotoa huduma katika Zahanati hiyo,, gari la kubrbea wagonjwa, na kuwataka wananchi kujiunga na mfuko wa BIMA ya Afya Iliyoboreshwa kwa gharama ya shilingi elfu 30 tu, ili kupata dawa na vifaa tiba katika zahanati hiyo.
Hata hivyo, wananchi wa kijiji cha Losinoni Juu, wamedhihirisha kufurahishwa na ujenzi wa Zahanati hiyo, na kuthibitisha kuwa changamoto ya vifo vya mama na mtoto vinavyosababishwa na ukosefu wa huduma za afya kwa karibu sasa imefikia kikomo, na kukiri kutumia zahanati hiyo kwa ajili ya kuokoa maisha yao.
Mama Sara, mkazi wa kijiji cha Losinoni Juu, amesema kuwa, kinamama wajawazito wamekuwa wakitembea umbali mrefu kupata huduma za kliniki na kujifungua, jambo ambalo lilisababisha, wajawazito kujifungulia njiani na wengine kupoteza maisha huku wazazi wengi wakishindwa kuwapeleka watoto wao kliniki kwa utaratibu uliopangwa.
"Kutokana na umbali, wazazi wengi hawawapeleki watoto kliniki, wajawazito hushindwa kuhudhuria kliniki, wengi kujifungulia nyumbani, na inapotokea tatizo la kupekwa hospitali hujifungulia njiani na wengine kupoteza maisha ya mama na mtoto" amethibitisha mama Sara.
Zahanati hiyo imejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 56 na kufanya halmashauri ya Arusha kufikisha jumla ya Zahanati 48, Vituo vya afya 7 na hospitali 2, lengo kubwa likiwa ni upatikanaji wa huduma na afya pamoja na dawa zote za msingi, ili kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.