Wananchi wa kijiji cha Loovilukuny kata ya Kisongo, halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru, wameondokana na adha ya uhaba wa maji, iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu, mara baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji katia kijiji chao.
Wananchi hao wamefurahishwa na neema kubwa ya maji, ambayo kwa sasa yameanza kupatikana katika maeneo yao, tofauti na hapo awali ambapo iliwalazimu kutembea umbali mrefu kwenda vijiji vya jirani kupata huduma ya maji.
Wameongeza kuwa, adha ya maji ilikuwa inawakabili kijijini hapo, ilikua ikizorotesha maendeleo ya kijiji chao, jambo ambalo liliwafanya kutumia muda mwingi kutafuta maji huku wanawake na watoto, wakiteswa zaidi na adha hiyo.
Hata hivyo wananchi hao, wameishukuru Serikali ya awamu ya tano, huku wakimpongeza zaidi Rais John Pombe Magufuli kwa kasi yake ya uchapaji kazi, inayosababisha upatikanaji wa huduma muhimu za jamii hadi kwa wananchi wa vijijini.
Nasinyari Mollel mkazi wa kitongoji cha Loongululu, amesema kuwa, wamefurahi sana kupata maji katika maeneo yao, kwani wao kama wanawake walikuwa wanateseka sana na kulazimika kutumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya shughuli nyingine za kujiongezea kipato.
" Kwa kweli tunaishukuru Serikali kwa kutupunguzia mateso sisi wanawake, tulikuwa hatufanyi kazi zaidi ya kutafuta maji, siku ya kuchota maji hakuna kazi nyingine, lakini sasa Hapa Kazi tuu" amesema mama huyo
Mhandisi wa maji, halmashauri ya Arusha, Mhandisi Christina Kessy, amethibitisha kukamilika kwa mradi huo kwa zaidi ya asilimia 90%, na kuongeza kuwa tayari vituo 19 vya kuchotea maji vimeanza kutumika na wananchi wanapata huduma ya maji katika vituo hivyo.
Ameendelea kufafanua kuwa, mradi huo wa maji Loovilukuny ni miongoni mwa miradi ya maji ya vijiji kumi, uliyoulianza rasmi mwaka 2013, kupitia miradi ya mkopo ya Benki ya dunia na kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.03, mradi ambao utahudumia takribani watu 4,750 wa kijiji hicho na vitongoji vyake.
Aidha Mhandisi Kessy amewataka wananchi wa kijiji hicho, kufahamu kuwa mradi huo ni mali yao, hivyo wanapaswa kushirikiana kwa pamoja kutunza miundombinu yote ya maji, kuanzia kwenye matenki, mabomba yaliyopitishwa kwenye maeneo yote pamoja na vituo vyote vya kuchotea maji.
“Ili mradi huu uwe endelevu, ni jukumu lenu wananchi kufahamu mradi huu ni wenu na si wa serikali tena, kazi yenu kubwa ni kulinda na kuitunza miundombinu yote ya maji ili msirudi tena kwenye adha ya maji mliyokuwa mkiipata”. Amesisitiza Mhandisi huyo.
Kukamilika kwa mradi wa maji wa Loovilukuny, kumetimiza idadi ya miradi ya vijiji kumi, na kufikia miradi mitano ilyokamilika,ambapo miradi mingine ni mradi wa maji Nduruma, Ilkerevi, Oloigwenino na Ngaramtoni huku miradi mingine ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezwaji.
Wananchi wa kitongoji cha Loovilukuny wakichota maji kwenye moja ya vituo vya kuchotea maji, mara baada ya mradi wa maji Loovilukuny kukamilika na kuanza kutumika.
Wanawake wa Kitongoji cha Loongululu wakichota maji huku wakifurahia upatikanaji wa huduma ya maji karibu na maeneo yao.
Kituo cha kunyweshea mifugo kitongoji cha Lovilukuny, hii ni miongoni mwa huduma inayokwenda sambamba wakati wa utekelezaji wa miradi ya maji katika maeneo ya wafugaji.
Moja ya kituo cha kuchotea maji, Loovilukuny
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.