Na. Elinipa Lupembe.
Wanachi wa kijiji cha Olchorovus kata ya Musa, wameiomba serikali kupitia halmashauri yao ya Arusha, kuwasaidia umaliziaji wa mradi wa ujenzi zahanati ya Olchorovus pamoja na nyumba ya mhudumu wa afya, miradi ambayo wameijenga na tayari imekamilika kwa asilimia 80%.
Wananchi hao wamefikia hatua hiyo kutokana na mateso wanayoyapata, pindi wanapougua na kulazimika kutembea umbali mrefu ili kupata huduma za afya, jambo ambalo linalosababisha vifo vya mara kwa mara, vinavyotokana na kukosa huduma za afya kwa wakati.
Akizungumza na mwandishi wetu diwani wa kata ya Musa Mhe. Florah Zelothe, amesema kuwa, wananchi wa Olchorovus wamekuwa wakitembea umbali wa zaidi ya Kilomita 15, kufuata huduma za afya, kwenye hospitali ya wilaya ya Oltrumet kata ya Olturumet, jambo linalowasababishia usumbufu mkubwa, pamoja na vifo, hususani kwa wananwake wajawazito na watoto wakati wa kujifungua.
Mheshimiwa Florah ameongeza kuwa, wajawazito wengi wanashindwa kuhudhuria kliniki pamoja na kujifungulia nyumbani kutoka na umbali wa hospitali jambo ambalo ni hatari kwa afya zao.
Aidha amethibitisha kwa mwaka uliopita 2018, wanawake wajawazito wapatao watatu walipoteza maisha wakati wa kujifungua na kuacha simanzi na maumivu kwa familia, huku wengine wakijifungua watoto njiti kwa kukosa elimu ya afya ya uzazi wakati wa ujauzito na kuongeza kuwa, uwepo wa zahanati hiyo utasaidia kupunguza vifo hivyo, wajawazito kuhudhuria Kliniki na kuacha tabia ya kujifungulia nyumbani.
“Mwaka jana tumepoteza akina mama wajawazito watatu wakati wa kujifungua, kutokana na huduma kuwa mbali, mmoja alipatwa na kifafa cha mimba na mwingine kuchanika mfuko wa kizazi, kwa kushindwa kuwafikisha hospitali kwa wakati kutokana na umbali”. amesema diwani huyo.
Kwa upande wa mtendaji wa kijiji cha Olchorovus na kaimu mtendaji wa kata ya Musa Asheli Kiseri amesema, miradi hiyo imechukua muda mrefu, licha ya jitihada za kukamilisha ujenzi kufanyika lakini wananchi wameshindwa kuchangia kwa wakati, hususani kipindi wanaposhindwa kupata mazao, kwa kuwa wengi wao hutegemea kipato kutokana na shughuli za kilimo na ufugaji.
Hata hivyo, Afisa Mipango halmashauri ya Arusha, Anastazia Tutuba, amesema kuwa, halmashauri imeweka kwenye bajeti kiasi cha shilingi milioni 10, ambazo zitawezesha umaliziaji na ukamilishaji wa majengo hayo na kuleta watalamu wa afya ili kuwezesha Zahanati ianze kazi ya kuwahudumua wananchi wa kijiji cha Olcholovos.
Afisa Mipango huyo amewashauri wananchi wote, kuweka mikakati ya kuanzisha miradi na kuikamilisha, ili kuondokana na changamoto ya miradi viporo, na kusisitiza kuwa kipaumbele cha serikali kwa sasa kuanzisha miradi mipya na kuisimamia mpaka kukamilika na si kumalizia miradi ya nyuma.
Jengo la Zahanati ya Olchorovus kata ya Musa
Nyumba ya Mtumishi wa Zahanati ya Olchorovus kata ya Musa
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.