Na. Elinipa Lupembe
Wananchi Halmashauri ya Arusha Jimbo la Arumeru Magharibi, wameendelea kujitokeza kuhakiki taarifa zao, mara baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuweka wazi Daftari la Awali la Wapiga kura zoezi ambalo liko kwenye siku ya tatu kati ya siku nne za Zoezi hilo, kuanzia tarehe 17- 20/06/2020.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Moses Joel Hharty, mkazi wa kijiji cha Engorika kata ya Kiutu, alipokutwa na mwandisgu wetu akihakiki na kukagua taarifa zake leo, kwenye Ofisi za Makao makuu ya Halmashauri hiyo eneo la Sekei.
Hharty amesema kuwa, amelazimika kufika kituoni hapo kuhakiki taarifa zake, na kupiga picha upya mara baada ya kadi yake ya awali kuvunjika.
Aidha ameongeza kuwa, zoezi hilo limempa uhakika wa kushiriki kupiga kura katika uchaguzi mkuu, uchaguzi unaotarajia kufanyika mwezi Oktoba 2020, wa kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani.
"Nimefurahi sana kupata fursa ya kuhakiki na kupata kitambulisho kipya, kwani nilikuwa na hofu ya kuto kupiga kura mwaka huu kwa kukosa kadi ya kupigia kura, leo nina imani kura yangu ya kumchagua rais wangu iko salama"amesema Hharty.
Afisa Uchaguzi Hamashauri ya Arusha, Hadija Mkumbwa amesema kuwa, zoezi hilo linakwenda vizuri na limeweza kutatua changamoto mbalimbali za wapiga kura ikiwemo, kurekebisha majina, jinsia, tarehe, mwezi na mwaka wa kuzaliwa, kutoa kadi kwa waliopoteza na kuharibika kwa kadi zao.
Aidha Afisa Uchaguzi huyo, amewataka wananchi kutumia fursa hiyo adhimu,iliyotelewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kuhakiki taarifa zao, ili waweze kushiriki kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu wa 2020 kwa kuwa kura ni haki ya kila mtanzania mwenye sifa.
"Mwananchi aliyejiandikisha anatakiwa kutumia fursa hii, kwenda kwenye kituo chake alichojiandikishia kupiga kura na kuhakiki taarifa zake, endapo atakuta taarifa zake si sahihi, aje ofisi za halmashauri yetu eneo la Sekei, kufanya marekebisho, pamoja na wale waliopoteza kadi zao na wale ambao kadi zao zimeharibika, waje watapata kadi mpya, zoezi litamalizika kesho" amesema Afisa Uchaguzi huyo.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.