WANANCHI WATAKIWA KUTOA MAONI KUBORESHA SERA ZA KODI NA UWEKEZAJI
Wananchi na wadau wengine kutoka ndani na nje ya nchi wametakiwa kutumia fursa iliyotolewa na Serikali, ya kutoa maoni na kuwasilisha mapendekezo yao ya kuboresha sera za kodi kwa kuwa Serikali inaendelea kupokea maoni hayo ili kukuza uchumi wa nchi.
Rai hiyo ilitolewa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, wakati akizungumza na Wadau wa sekta wa Habari, katika Ofisi za Hazina Ndogo, jijini Arusha ikiwa zimebaki siku chache kuelekea Kongamano la Pili la Kodi na Uwekezaji , litakalofanyika Jijini Dar es Salaam tarehe 15 April, 2025.
Alisema kuwa kuanzishwa kwa Kongamano la Kodi kumeleta tija katika maboresho ya mfumo wa kodi ambapo katika maandalizi ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ushirikishwaji wa wadau uliongezeka zaidi huku ukileta manufaa mbalimbali kiuchumi.
‘’Wakati tunaanza Kongamano hili, chini ya Serikali inayoongozwa na Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mwaka 2022, kupitia sera mbalimbali tulizorekebisha, miradi zaidi ya 293 ilisajiliwa na Kituo chetu cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mwaka, 2023, miradi zaidi ya 526 ilisajiliwa, mwaka 2024 ambapo miradi zaidi ya 901 ilisajiliwa pia’’ alisema Bw. Mwandumbya.
Alieleza kuwa, mapato ya ndani kwa mwaka 2022/23 yalikuwa shilingi trilioni 26.3, mwaka 2023/2024 yalikuwa shilingi trilioni 29.8 sawa na ongezeko la asilimia 13.5.
Aidha, alisema kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai 2024 hadi Februari 2025 mapato ya ndani yalikuwa shilingi trilioni 22.579.
Aliongeza kuwa Kogamano la Kodi Kitaifa kwa mwaka huu, linatarajiwa kuwashirikisha wadau mbalimbali zaidi ya 1,000 kama sehemu ya walengwa wa masuala ya kodi na uwekezaji ili kuendelea kuboresha mfumo wa kodi kwakuwa lengo ni kukuza uchumi wa nchi na wananchi kwa ujumla.
"Kazi yetu ni kuwafikia wananchi, wafanyabiashara na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kuwa tunakusanya maoni yatakayofaa kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu, azma ambayo tumeona ni vyema kuichukua kwa mwaka huu, tunalenga kuongeza ukuzaji wa rasilimali za ndani kwa kustawisha fursa za wananchi’’ alisema Bw. Mwandumbya.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.