Na Elinipa Luoembe
Jumla ya watoto 88, 628 wenye umri wa chini ya miaka 5, wanategemea kupatiwa chanjo ya matone dhidi ya ugonjwa wa Polio kwa awamu ya tatu, inayotegemea kufanyika kwa siku 4, kuanza tarehe 01 - 04 Septemba 2022.
Akizungumza wakati wa kikao cha Maandalizi ya Kampeni ya Chanjo ya Polio ngazi ya wilaya, mkuu wa wilaya ya Arumeru, Mhandisi Richard Ruyango amewasisitiza wazazi na walezi kuhakikisha wanawapeleka watoto wenye umri huo kupata chanjo hiyo muhimu kwa ajili ya kuokoa maisha yao.
Mkuu huyo wa wilaya, amewataka watoa huduma wote kuhakikisha wanatoa chanjo hizo kwa wakati, pindi wazazi watakapofika kwenye vituo hivyo vya afya kupata huduma hizo.
Mganga Mkuu halmashauri ya Arusha, Dkt. Petro Mboya, ameweka wazi kuwa, ugonjwa wa Polio hauna dawa ila una kinga, na kundi la watoto wa chini ya miaka 5 wako kwenye hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa Polio, ugonjwa ambao husababisha kupooza na kusababisha ulemavu wa kudumu na pengine kifo.
"Hata kama mtoto amepata chanjo zote za Polio, anatakiwa kwenda kuchanja, na hata kama mtoto yuko kwenye chanjo anatakiwa akapate chanjo hiyo na aendelee na ratiba ya kupata chanjo kama kawaida". Amesisitiza Dkt. Mboya.
Mratibu wa Chanjo, halmashauri ya Arusha, amebainisha kuwa, Idara yaAfya imepjipanga kuhakikisha wanawafikia watoto wote, walio kwenye maoteo na kufikisha asilimia zaodi ya 100 kwa kuwatumia watoa huduma kuwafuata watoto nyumbani.
Jumla ya Vituo 59 vya halmasahuri ya Arusha, vitatumika kutoa chanjo hiyo ya Polio kwa siku zote 4, baadhi ya maeneo kupitia huduma za mkoba (mobile clinic) pamoja na kampeni ya nyumba kwa nyumba.
Kampeni ya Chanjo ya Polio yenye kauli mbiu ya Mpe chanjo,Okoa Maisha, inatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wafadhili wa shirika la Watoto UNICEF pamoja na shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lengo likiwa kuokoa maisha ya watoto.
Awali katika kampeni ya chanjo ya Polio awamu ya pili jumla ya watoto 86,053 walipata chanjo sawa na asilimia 149.3.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.