Na .Elinipa Lupembe.
Watumishi wa Umma wametakiwa kupanga namna ya kupata lishe bora wawapo kazini, kwa kuhakikisha wanapata chakula chenye virutubisho vinavyotokana na makundi matano ya vyakula kutokana na muda wao wa kula kuwa finyu kutokana na mazingira halisi ya muda wa kazi.
Hayo yamesemwa na Mganga mkuu wa Jiji la Arusha, Dkt. Kheri Kagija wakati akifunga mafunzo ya Afya katika sehemu za kazi, yaliyowakutanisha wawakilishi wa kamati za Lishe, Maafisa Lishe na Maafisa Ugani wa halmashauri za mkoa wa Arusha, kikao kilichofanyika kwenye hoteli ya Safari ya Jijini Arusha.
Dkt. Kagija amefafanua kuwa, maendeleo ya taifa lolote, yanawategemea wafanyakazi, ambao wantumia nguvu nyingi kufaya kazi, nguvu ambazo zinategemea afya bora, hivyo ni vema wafanyakazi wakapata chakula bora, chenye virutubisho vyote vinavyotkana na makundi matano ya chakula kila mlo wanaoupata wawapo kazini.
Aidha Dkt. Kagija amewataka Maafisa Lishe wa halmashauri zote kutoa elimu kwa wafanyakazi, itakayowawezesha kuwa na ratiba nzuri ya chakula katika maeneo yao ya kazi, chakula chenye virutubisho vyote lengo likiwa ni kunusuru afya za watumishi wa Umma.
Ameweka wazi kuwa ulaji wa wafanyakazi wawapo kazini, umekuwa ni chanzo cha kudhoofisha sana afya zao na kujikuta wengi wao, wakishambuliwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo, kisukari, shinikizo la damu, vitambi, baridi yabisi pamoja na utapiamlo uliozidi bila kufahamu maradhi hayo yanatokana na ulaji mbovu wanoufanya wawapo kazini.
"Ni kawaida kukuta mfanyakazi asubuhi anapata supu chapati na soda, chai chapati ama maandazi, kwa wiki nzima, huku mchana akilazimika kula ugali ama wali nyama, chipsi mayai na mishikaki ama nyama choma na ndizi, vyakula ambavyo kwa asilima kubwa vinaangukia kwenye kundi moja ama mawili tuu ya vyakula" amefafanua Dkt. Kagija.
Naye Meneja Mkuu wa Mradi wa shirika la Global Alliance for Improved Nutrition 'GAIN' Dkt. Winfrida Mayilla, ameongeza kuwa ni vema kutoa elimu ya lishe kwa wafanyakazi kwa kuwa wanatumia muda mwingi kazini huku ratiba zao za kula zikiathiriwa na muda na mazingira, kupitia elimu ya lishe, wafanyakazi wanaweza kujenga tabia ya kupata chakula chenye virutubisho, jambo ambalo litaimarisha afya za wafanyakazi.
"Wafanyakazi wanatakiwa kuzingatia ulaji mzuri wa chakula, chakula ambacho kitakuwa ni mlo uliobeba virutubisho vinavyotoka na makundi yenye mchanganyiko wa nafaka, matunda, wanyama na mikunde, mbagamboga na mafuta." Amesema Dkt. Winifrida.
Hata hivyo washiriki wa mafunzo hayo, wakiwemo Maafisa Lishe, wamethibitisha ulaji mbovu wa watumishi wawapo kazini, kutokana na kutumiamjuda mrefu kazini na kukosa muda wa kuandaa chakula chenye virutubisho vinavyotokana na makundi matano ya chakula, na kujikuta wakila vyakula vya aina moja kwa muda mrefu, jambo linalowasababishia kuwa na afya duni
Afisa Lishe halmashauri ya Arusha, Doto Milembe, amethibitisha kuwepo na tabia hasi za ulaji kwa wafanyakazi kutokana na uelewa mdogo wa masuala ya ulaji, na kuongeza kuwa wanajukumu la kutoa elimu kwa watumishi pamoja na kuwapima uzito mara kwa mara, ili waweze kujua afya zao na kuanza kula chakula chenye virutubisho vyote wawapo kazini.
Mafunzo hayo ya siku moja yamekutanisha maafisa Lishe,maafisa Ugani, maafisa Afya pamoja na na wajumbe wa kamati za Lishe kutoka halamshauri saba za mkoa wa Arusha.
Arusha
Kazi inaendelea✍✍
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.