Na. Elinipa Lupembe.
Wawakilishi wa Vyama vya siasa vitakavyoshiriki Uchaguzi Mkuu, Jimbo la Arumeru Magharibi wamekutana na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Arumeru Magharibi na kufanya kikao, kwa ajili ya kupeana taratibu za mchakato mzima wa Uchaguzi Mkuu, unaotarajia kufanyika tarehe 28 Oktoba, 2020.
Katika kikao hicho, kilichofanyika kwenywe Ofisi ya Uchaguzi halmashauri ya Arusha, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Arumeru Magharibi, Saad Mtambule, amewataka wawakilishi hao wa Vyama vya Siasa kuzingatia Kanuni, sheria na taratibu zinazoelekezwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ambao ndio msingi wa uchaguzi ulio huru na haki.
Amefafanua kuwa, miongozo ambayo imeandikwa kwenye vitini vilivyoandaliwa na Tume na kugawiwa kwa wawakilili wa vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, imelenga kuwa na uchaguzi huru, haki, uwazi na kuaminika, wenye kuzingatia ushiriki wa makundi wa makinsi yote ya jamii na watanzania wote
Mtambule amewasisitiza Wawakilishi hao wa vyama vya siasa, kushirikiana na Tume ya Uchaguzi, kuwaelimisha wananchi hasa wafuasi wa vyama vyao, kufahamu haki na wajibu wao katika uchaguzi mkuu, ili kuwa na uelewa wa pamoja, utakaowezesha uchaguzi kuwa wa amani, huru na wa haki.
"Ili Uchaguzi Mkuu uwe wa amani, ni jukumu letu wasimamizi wa Uchaguzi na ninyi wawakilishi wa vyama na wafuasi wa vyama vyenu kujenga nidhamu na kuheshimu taratibu zinavyoelekeza, waelimisheni wanachama wenu kutambua hilo kipindi chote cha Uchaguzi, ili Uchaguzi uwe wa amani kwa maslahi ya watanzania wote" amesisitiza Mtambule.
Aidha amawataka wawakilishi hao wa vyama, licha ya kufuata kanuni na taratibu, amewakumbusha kuzingatia ratiba waliyokabidhiwa, waweze kuendana na muda na matukio yaliyoelekezwa kwa wakati husika, lengo likiwa kuepuka malalamiko yasiyokuwa ya lazima katika kipindi chote cha Uchaguzi.
Hata hivyo wajumbe hao wamekubaliana kufanya mchakato wa uchaguzi kwa amani na utulivu na kuweka maslahi ya watanzania mbele, huku wakimuomba Msimamizi wa Uchaguzi, kusimamia uchaguzi uwe huru na haki, huku wakisisitiza kuwa maisha ya watanzania ni zaidi ya uchaguzi kwa kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi.
Awali Wawakilishi hao wa Vyama vya Siasa, wamekabidhiwa vitini vya miongozo mbalimbali ya Uchaguzi Mkuu pamoja na Ratiba ya mchakato mzima wa Uchaguzi kama ilivyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.