Na Elinipa Lupembe
Wazazi wametakiwa kuhakikisha wanawahudumia watoto wao wa shule za kutwa kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa wa kuwapa chakula cha mchana watoto wao wawapo shuleni.
Rai hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Arumeru Mhe. Emmanuela Mtatifikolo Kaganda, wakati akizundua jengo la maabara za masomo ya Sayansi Fizikia na Kemia shule ya sekondari Oldonyowas na kutembelea bwalo la chakula shuleni hapo.
Mhe. Emmanuela amesema kuwa Serikali imeshatekleza jukumu lake la kuwekeza kwenye miundo mbinu ya shule hivyo ni jukumu wanafunzi kusoma kwa bidii, huku akiwataka wazazi kuwawezesha watoto hao kusoma vizuri kwa kuwapa chakula cha mchana.
"Sera ya Elimu bila malipo imeweka wazi majukumu ya mzazi kumhudumia mtoto wake kwa kumpatia mahitaji yake muhimu ikiwemo vifaa vya shule,madaftari, nguo za shule, usafiri pamoja na chakula cha kwa shule zisizo za bweni, chakula cha mchana kwa wanafunzi wa shule za kutwa, hivyo wazazi msikwepe jukumu hilo ni lenu"Amesisitiza Mkuu huyo wa wilaya.
Aidha amefafanua kuwa ni jukumu la mzazi kumpa mtoto chakula, zaidi chakula ni haki ya msingi ya mtoto na ni muhimu kwa afya yake pia, na kuongeza kuwa ili mtoto aweze kusoma na kufaulu vizuri lazima awe na afya njema inayotokana na lishe bora, lazima awe ameshiba ili aweze kufaulu vizuri.
Hata hivyo mwanafunzi wa kidato cha III, Godfrey Mbise amewataka wazazi kuona umuhimu wa kuwachangia chakula watoto wao, kwa kuwa wapo watoto ambao hawali shuleni jambo ambalo linawatia unyonge na kushindwa kufanya vizuri kwenye masomo yao.
"Serikali imefanya vizuri kutuwekea mazingira bora ya kusomea, changamoto kubwa ni bado kuna baadhi ya wazazi wanashindwa kuwalipia watoto wao chakula, jambo ambalo linawafanya kushinda njaa, niwaombe wazazi kuwahurumia watoto wao, ili mwanafunzi aweze kuconcentrate kwenye masomo lazima awe ameshiba" Amesisitiza Godfrey
ARUSHA DC NI YETU, TUSHIRIKIANE KUIJENGA
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.