Na.Elinipa Lupembe.
Wazazi na walezi, halmasahuri ya Arusha, wametakiwa kuhakikisha wanawapeleka watoto wao wenye umri wa chini ya miaka 5, kupata chanjo dhidi ya ugonjwa hatari wa polio.
Rai hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi halmashauri ya Arusha, na Mkuu wa Idara ya Utumishi, Elizabeth Ngobei, wakati wa uzinduzi zoezi la chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio, uzinduzi uliofanyika kwenye zahanati ya Moivo, kata ya Moivo, katika halmashauri hiyo
Kaimu Mkurugenzi huyo, amewasisitiza wazazi wenye watoto wa umri huo, kuhakikisha wanapata chanjo dhidi ya ugonjwa hatari wa polio, kupitia zoezi la Kitaifa la chanjo ya Polio, zoezi linakalofanyika kwa muda wa siku nne kuanzia tarehe 18 - 21 Mei 2022, kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya pamoja na huduma mkoba kwa baadhi ya maeneo.
Aida amefafanua kuwa ugonjwa wa polio hutokana na virusi ambavyo huambukizwa zaidi kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, na watu ambao hawajapa chanjo, na zaidi husambazwa kwa njia ya kugusana na mtu aliyeambukizwa, kupitia kamasi na kinyesi chenye maambukizi.
"Ugonjwa wa polio hauna tiba maalumu zaidi ya chanjo inayozuia kupata maambukizi, niwatake wazazi na walezi kutumia fursa hiyo kuwapa kinga watoto, kwa kuwa virusi hivyo vya polio, huathiri mfumo wa neva na kusababisha udhaifu wa misuli, na matokeo yake mtoto hupooza" amesisistiza Kaim Mkurugenzi Elizabeth
Naye Mganga Mkuu wa halmashauri ya Arusha Dkt. Petro Mboya, amesema kuwa katika zoezi hilo la kitaifa, halmashauri ya Arusha inategemea kuchanja jumla ya watoto 57,673, huku zoezi hilo likifanyika kwa muda wa siku 4.
Dkt. Mboya, ameweka wazi kuwa, zoezi hilo cha chanjo ya polio, limeanza vizuri huku wazazi wenye watoto wa umri huo, wakionesha muitikio mkubwa, kwa kujitokeza kwenye maeneo ya kutolea huduma za afya, na kiwasisitiza wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao kupata chanjo hiyo.
Hata hivyo baadhi ya wazazi waliokutwa na mwandishi wetu, kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, wameishukuru serikali kwa kutoa chanjo hiyo ya polio, kwa kuwa wengi wao wamedai, kufahamu madhara ya polio kutokana na kuhadhithiwa na wazazi kwamba ugonjwa wa polio hauna dawa na husababisha mtoto kupooza.
Rachel Peter, mama wa mtoto Yese Peter mwenye umri wa mwaka 1 na miezi 4 na mkazi wa kijiji cha Losinoni, ni miongoni mwa mzazi, aliyempeleka mtoto wake kwenye zahanati ya Losinoni kupata chanjo ya polio, amethibitisha kuhadithiwa madhara ya ugonjwa wa polio na kuamua kumpeleka mtoto wake kupata chanjo ambayo anaamini itamkinga mtoto wake dhidi ya kupooza.
"Mimi sijawahi kuona mgonjwa wa polio, lakini nimehadithiwa na wazee, madhara yake, nikaogopa sana, na ndio maana leo siku ya kwanza tu, nimekuja kumleta mtoto wangu, wamama wengi unawaona hapa, wanafahamu madhara ya polio, hivyo tunaishukuru serikali ya mama Samia, kwa kuona umuhimu wa kutoa chanjo hiyo" amefafanua Rachel.
Mtabibu wa Zahanati ya Losinoni, Salum Litekelo, amethibitisha,kuwa zoezi la chanjo, limeanza vizuri, kutokana na wazazi kujitokeza kwa kupeleka watoto wao kupata chanjo hiyo.
"Licha ya kuwa leo ni siku ya kwanza na zoezi hili lilishatangazwa na kuahirishwa lakini limeanza leo na mwitikio wa wazazi unaridhisha, tunategemea watoto wote wa kijiji cha Losinoni Kati watapata chanjo hii" amesema Litekelo.
Ikumbukwe kuwa zoezi la chanjo ya Polio limetokana na mlipuko wa ugonjwa uliotokea katika nchi jirani ya Malawi, huku Tanzania ikipata mgonjwa wa mwisho wa polio mwaka 1996 na mwaka 2015, Tanzania ilipata cheti cha kutoka shirika la Afya Duniani cha kuonesha kutokuwa na mgonjwa polio.
#KaziIendeleeSHIRIKI
JIANDAE KWA SENSA YA WATU NA MAKAZI 2022.
'JITOKEZE KUHESABIWA 23 AUGOSTI 2022'✍✍
Kaimu mkurugenzi halmasahuri ya Arusha na mkuu wa Idara Utumishi, Elizabeth Ngobei, (wa pili kushoto) akimpatia matone ya polio mmoja wa watoto, ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa zoezi la chanjo Kitaifa, uzinduzi uliofanyika kwenye zahanati ya Moivo.
Mtabibu wa zahanati ya Losinoni kati, akimpa matone ya chanjo ya polio mtoto Yese Peter, aliyefika kwenye zahanati hiyo kupata chanjo ya polio.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.