Na Elinipa Lupembe
Wazazi na walezi wametakiwa kuamka na kuanza harakati madhubuti za kupambana na ukatili wa kingono dhidi ya watoto wa kiume, kama inavyofanyika kwa watoto wa kike kwa kipindi kirefu sasa.
Rai hiyo imetolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii, Dawati la Jinsia, Rovil Nguyaine, wakati wa kikao kazi kilichojumuisha wajumbe wa Kamati ya MTAKUWWA ngazi ya kata kutoka kata 6 za halmashauri ya Arusha, kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.
Nguyaine amebainisha ongezeko la kasi la matukio ya ulawiti kwa watoto wa kiume, watoto ambao wazazi na jamii hawakushughulika nao kwa dhana ya kuwa wanao uwezo wa kujitetea kiume, jambo ambalo madhara yake yameanza kuonekana sasa.
Ameongeza kuwa ni jukumu la wazazi na jamii, kuhakikisha wanawalinda watoto wote dhidi ya ukatili wa kijinsia na sio watoto wa kike peke yao, kwa kuwa watoto wote ni sawa na wanahitaji kulindwa kuanzia nyumbani, njiani mpaka shuleni.
"Wazazi/ Walezi jengeni desturi ya kushirikiana na walimu katika kupambana na ukatili wa kijinsia, hakikisheni mnakuwa karibu na watoto wenu, kwa kuwa hali ya ukatili ni mbaya sana hasa kwa wtoto wa kiume". Amesema Ngutaine
Hata hivyo wajumbe hao wa kamati ya MTAKUWWA licha ya kushukuru kikao kazi hicho, wamethibitisha uwepo wa matukio ya ukatili kwa watoto wa kiume na kuahidi kuendelea kuhamisisha jamii kujikita kupambana na ukatili kwa watoto wote wa kike na wa kiume.
Wameongeza kuwa, kupitia mafunzo wanayopewa na serikali na mashirika juu ya ulinzi na usalama wa watoto, umewezesha jamii kuanza kuwa na uelewa wa pamoja juu ya usimamizi wa usalama na haki za watoto, sambamba na namna ya kushughulikia matukio ya ukatili pindi yanapotokea.
Naye mjumbe wa Kamati ya MTAKUWWA kata ya Moivo Elizabeth, amelilalamikia jeshi la Polisi kuwa na vikwazo wakati wa ufuatiliaji wa kesi za ukatili na kuweka wazi kuwa, kutokana na ukiritimba uliopo, unasababisha wengi kurudi nyuma kwa kukataa tamaa kutokana na usumbufu.
Hata hivyo Mratibu wa Dawati la Jinsi, na Mpelezi wa kesi za Ukatili, Kituo cha Polisi Ngaramtoni, Koplo Jane Mandi amewataka wazazi na wajumbe wa MTAKUWWA kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa matukio yoyote ya ukatili pamoja nakufuata taratibu ambazo zitawezesha kesi kufika mwisho na hatimaye watoto kupata haki zao.
"Jeshi la Polisi liko tayari kushirikiana na kamati za MTAKUWWA kwa matukio yote ya ukatili na kuhakikisha watuhumiwa wanatiwa hatiani na kujitoa kutoa ushahidi kwenye kesi ili watoto waweze kupata haki zao, kwa sasa Jeshi la Polisi linasimamia kwa uwazi haki za watoto.
Koplo Jane amezungumzia mila na desturi za jamii bado ni kikwazo cha kesi nyingi za ukatili kutoka na ukweli kwamba matukio hayo yanatokea ndani ya familia na kusababisha wahanga kuogopa kutengwa na familia zao.
Awali Mratibu wa Mradi wa Kupinga Ukatili wa Kingono dhidi ya Watoto wa kiume, Shirika la CWCD, Mariam Rashid amesema kuwa lengo la kikao kazi hicho ni kukumbushana majukumu kwa wajumbe wa kamati ya MTAKUWWA na kuwashirikisha kushiriki mradi wa ukatili wa kingono kwa wavulana unaonedelea kwenye kata zao.
Halmashauri ya Arusha kwa kushirikiana na shirika la Center for Women and Children Develepment ( CWCD), wanatekeleza mradi wa kupinga ukatili wa kingono kwa watoto wa kiume kwenye kata 6, kwa ufadhili wa Foundation for Civil Society.
ARUSHADC
KaziIendelee✍
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.