Na. Elinipa Lupembe.
Wazee halmashauri ya Arusha, wameungana na wazee wote, kuadhimisha siku ya Wazee Duniani, huku jumla ya wazee 11, 076 wakiwa tayari wana vitambulisho vya matibu ya Wazee, maadhimisho yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano, halmashauri ya Arusha.
Taarifa hiyo imethibitishwa na mgeni rasmi na mkuu wa wilaya ya Arumeru, Mheshimiwa Mhandisi Richard Ruyango, kuwa wazee wa halmashauri hiyo, wameadhimisha siku hiyo maalum kwao, wakati halmashauri ikiwa imefanikiwa kuwawezesha jumla ya wazee 11, 076 kati ya wazee 12,892 waliotambuliwa.
Mkuu wa wilaya Ruyango amefafanua kuwa, serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu Hassan, inatambua thamani kubwa ya wazee waliotumikia taifa la Tanzania katika kipindi cha maisha yao, zaidi inatambua mchango wa wazee katika maendeleo ya Taifa hili, hivyo inaendelea kuboresha miundombinu ya huduma kwa wazee, na kuhakikisha wazee wanaendelea kupata huduma bora, lengo likiwa ni kuwafanya kuendelea kuishi kwa amani na utulivu, huku wakifurahia matunda ya nchi yao.
Aidha mkuu huyo wa wilaya amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wazee, kwa kuwepo na dirisha maalumu la kutibiwa wazee kwenye kila kituo cha kutolea huduma za afya, ili kuwaharakishia upatikanaji wa huduma za matibabu, mara wazee wanapofika kwenye kituo vya afya.
"Mkurugenzi na Mganga mkuu, hakikisheni kila kituo cha afya kuna dirisha la Wazee, lakini ikiwezekana apangwe muhudumu wa afya, maalumu wa kuwahudumia wazee, pindi wanapofika kupata matibabu, ili wasikae muda mrefu wakati wa kupata huduma za matibabu". Amesisitiza Mheshimiwa Ruyango.
Hata hivyo wazee hao wamewasilisha changamoto zinazowakabi ikiwa ni pamoja na kulea wajukuu ambao ni yatima na wengine kutelekezwa na wazazi wao, pamoja na baadhi ya wazee wasiokuwa na vitambulisho vya matibabu ya wazee kukosa matibabu pindi wanapougua, pamoja na Viongozi wa Baraza la wazee kutokuwa na ofisi maalum ya kuwahudumia wazee.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wazee halmashauri ya Arusha, Mzee Elias Ngungati amemshukuru mkuu wa wilaya ya Arumeru kupitia ofisi ya mkurugenzi na watalamu wa halmashauri ya Arusha kwa kuwajali wazee, pamoja na changamoto zinazowakabili wazee, lakini halmashauri imeendelea kuboresha maslahi mbalimbali ya wazee kupitia Baraza la wazee la halmashauri mpaka kuwafikia kwenye ngazi ya kata.
"Licha ya kuwa bado kuna changamoto zinazowakabili lakini serikali inaendela kufanya maboresho tofauti na hapo awali, na kusisitiza kupewa ofisi ya viongozi wa Baraza la Wazee ili kurahisiha upatikani wa viongozi pindi wazee wanapotaka kukutana na kujadili mambo yao" amesisitiza Mwenyekiti Ngungati.
Awali mkurugenzi mtendaji halmashauri ya Arusha Seleman Msumi, amekiri kutambua na kupokea changamoto zilizowasilishwa na wazee hao, na kuahidi kuzifanyia kazi na kutatua baadhi ya kero hizo kwa awamu, kulingana na upatikanaji wa fedha na kusisitiza kusimamia upatikanaji wa huduma za haraka za afya kwa wazee, kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya pamoja na kutafuta namna ya kuwapatia viongozi wa Baraza la Wazee ili kurahisisha ukutanaji wao.
"Ninatambua changamoto za wazee ni nyingi, lakini halmashauri inaendelea kuzitatua na kuzipunguza kwa awamu, sambamba na kupatikana kwa ofisi za uongozi wa Baraza la Wazee" amesistiza mkurugenzi Msumi.
Katika maadhimisho hayo, idara ya Afya ilifanikiwa kutoa elimu ya ugonjwa hatari wa Covid 19 (UVIKO 19) kwa kuwataka wazee kupata chanjo ya UVIKO19 pamoja na kuendela kujihadhari na ugonjwa huo hatari.
Maadhimisho hayo ya siku ya Wazee Duniani hufanyika tarehe 01, Oktoba kila mwaka, huku halmashuri ya Arusha, ikiadhimisha kwa kuhusisha Baraza la Wazee pamoja na Wazee wawakilishi kutoka kata zote 27 za halmashauri ya Arusha, maadhimisho hayo yamefanyika kwa ushirikiano wa halmashuri na wadau wa maendeleo wa shirika la DORCAS na CWCD, yakiwa na kauli mbiu Mbiu ya siku ya Wazee 2021: "MATUMIZI SAHIHI YA KIDIGITALI KWA USTAWI WA RIKA ZOTE"
MATUKIO KATIKA PICHA.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, mheshimiwa mhandisi Richard Ruyango akizungumza na wazee, wa halmashauri ya Arusha wakati wa maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani, maadhimisho yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano, halmashauri hiyo.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee, halmashauri ya Arusha, akisoma risala ya Wazee, mbele ya mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, mheshimiwa mhandisi Richard Ruyango wakati wa maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani, maadhimisho yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano, halmashauri hiyo.
Baadhi ya Wazee halmashauri ya Arusha, wakifuatilia mijadala mbalimbali wakati wa maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani, maadhimisho yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano, halmashauri hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi, akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani, maadhimisho yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano, halmashauri hiyo.
Baadhi ya Wazee halmashauri ya Arusha, wakifuatilia mijadala mbalimbali wakati wa maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani, maadhimisho yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano, halmashauri hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, mheshimiwa mhandisi Richard Ruyango akikabidhiwa Rungu na Wazee wa halmashauri ya Arusha, ikiwa ni ishara ya kumtawaza kuwa mlezi wa Wazee, wakati wa maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani, maadhimisho yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano, halmashauri hiyo.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.