Na Elinipa Lupembe
Wazee halmashauri ya Arusha, wamehimizwa kushiriki vikao vya mabaraza ya wazee, kuanzia ngazi ya kata, lengo likiwa ni kutekeleza sera ya Taifa ya wazee ya mwaka 2003 na sera ya Afya ya mwaka 2007, zikiwa na lengo la kuhakikisha Ustawi wa wazee nchini, vikao ambavyo vitawezesha kuweka mipango thabiti ya kukabiliana na changamoto zao pamoja na kuimarisha uhusiano baina yao.
Rai hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi na Afisa Utumishi Mkuu, halmashauri hiyo, Elizabeth Ngobei, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani kiwilaya, sherehe zilizofanyika kwenye viwanja vya makao makuu ya halmashauri hiyo na kuwataka kufahamu kuwa vikao vya mabaraza ya wazee ni vikao halali kisheria.
Kaimu Mkurugenzi huyo amesema kuwa serikali imeandaa utaratibu wa kuunda mabaraza ya wazee kuanzia ngazi ya kata, ikiwa ni njia ya kukutana na kubaini changamoto zinazowakabili na kisha kuziwasilisha ngazi ya wilaya na hatimaye Taifa ili serikali iweze kuweka mipango ya kuzitatua changamoto hizo.
"Vikao ndio utaratibu halali na sahihi wa kuwasilisha mambo yenu kwa Serikali, Serikali hufanyia kazi maamuzi yatakayotokana na mihitasari ya vikao hivyo halali, vinginevyo mtaishia kulalamika na itakuwa ni vigumu kufahamu na kuzitatua changamoto zenu, hakikisheni mnafanya vikao hivyo kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa". Amesistiza Elizabeth
Aidha, wazee walioshiriki kwenye Maadhimisho hayo, wamekiri kutambua changamoto za kutokufanya vikao vya mabaraza na kuahidi, kuanza kutekeza wajibu huo, kwa kutambua kuwa ni fursa kubwa waliyopewa na Serikali yao.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wazee, halmashauri ya Arusha Mzee Aloyce Mollel, amekiri kuwepo kwa changamoto ya ufanyikaji wa vikao vya mabaraza ngazi ya kata, jambo ambalo linakwamisha utatuzi wa changamoto za wazee na kuahidi kufuatilia na kuhakikisha vikao hivyo vinafanyika kwa mujibu wa sheria.
"Wapo baadhi ya wazee wanaishi kwenye mazingira magumu, kutokana na umasikini uliokithiri wanakosa lishe bora na kuishi kwenye makazi duni, tukikutana kwenye vikao na kuweka mawazo yetu pamoja, tutapata namna bora ya kuwasaidia kutatua changamoto zetu na sio kulalamika". Amesema mzee Aloyce
"Wazee wenzangu, serikali inatujali, imetupa fursa ya kuwa na Mabaraza ya Wazee, tukutane tujadili na tupange mambo yetu, tusijifungie ndani, kukaa ndani tunajiongezea magonjwa, tutoke na kushughulisha miili na akili zetu, ni afya kwa kufanya hivyo itatuongezea siku za kuishi" Amesisitiza Ndekusura Mwenera kata ya Moivo
Hata hivyo wazee hao wamekiri kuwa, licha ya changamoto nyingi zinazowakabili, wameadhimisha siku hiyo, huku wakiwa na matumaini na serikali ya awamu ya sita kwa chukua hatua katika kuboresha huduma za afya sambamba na kuwatambua wazee na kuwapa vitambulisho vya wazee.
"Tunaishukuru serikali kwa kuweka utaratibu wa kuongeza bajeti ya dawa, uwepo wa dirisha maalum la matibabu kwa wazee, tunaiomba serikali kutusaidia dawa za magonjwa yasiyoambukiza yanayowakabili wazee". Amesema Rose Mollel
Halmashauri ya Arusha imeazimisha siku ya wazee duniani yenye kauli mbiu ya 2022 yenye Kauli Mbiu ya " Ustahimilivu na Mchango wa Wazee ni Muhimu kwa Maendeleo", ikiwa imefanikiwa kuwatambua wazee 12, 892 kwa ajili ya kupatiwa huduma, huku wazee 11,076 wakipatiwa vitambulisho vya wazee sawa na asilimia 100.
Maadhimisho hayo yaliambatana na burudani za muziki wa zamani, mashindano ya kucheza muziki na wazee kuelezea kumbukumbu muhimu katika masha yao, sambamba na wazee kupata huduma ya kupima afya kwa magonjwa yasiyoambukiza.
'Uzee na Kuzeeka, Hakuna wa Kukwepa'
PICHA ZA MATUKI SIKU YA MAADHIMISHO
Kaimu Mkurugenzi na Afisa Utumishi Mkuu, halmashauri ya Arusha, Elizabeth Ngobei, akihutubia wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani,sherehe zilizofanyika kwenye viwanja vya makao makuu ya halmashauri hiyo.
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wazee, halmashauri ya Arusha Mzee Aloyce Mollel, akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani,sherehe zilizofanyika kwenye viwanja vya makao makuu ya halmashauri hiyo.
Baadhi ya Wazee walioshiriki kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniami halmashauri ya Arusha
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.