Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za mheshiwa Selemani Jafo amewapongeza wananchi wa halmashauri ya Arusha kwa kuchangia kwa hali na mali miradi ya maendeleo katika maeneo yao, na kuwataka wananchi wengine kuiga mfano huo.
Waziri Jafo ametoa pongeza hizo baada ya kuridhishwa na kuguswa na ujenzi wa kituo cha afya cha Ilkurot kata ya Olkokola kilichojengwa kwa nguvu za wananchi kwa kuchangishana wao kwa wao.
Waziri Jafo amethibitisha kuridhishwa sana na wananchi wa halmashauri ya Arusha kuchangia ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo kisekta, na kudhihirisha kuwa michango hiyo huiongezea nguvu serikali yao kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.
"Ninaridhishwa sana na juhudi za wananchi wa halmashauri hii katika kuchangia miradi ya maendeleo, serikali inatambua na kuthamini juhudi zenu wananchi, kufuatia juhudi hizo, serikali imetoa shilingi milioni 500 za kumalizia ujenzi wa kituo cha Afya Nduruma na zimesimamiwa vizuri, kituo hicho kilianza kujengwa na wananchi wa Nduruma, hata kituo hiki cha Ilkurot serikali itaongeza nguvu hapa" amesema Waziri Jafo.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa kituo cha Afya Ilkurot mbele ya Waziri Jafo, Afisa Mtendaji wa kijiji Ilkurot, Charles Sikoi, amesema kuwa wananchi wa kijiji hicho wamechanga kiasi cha shilingi milioni 30 na kuanza ujenzi huo kutokana na adha ya upatikanaji wa huduma ya afya katika eneo hilo.
Ameongeza kuwa mpaka kukamilika kwa jengo hilo, zinahitajika jumla ya shilingi milioni 96.6 na mpaka sasa jengo hilo limetumia shilingi milioni 29 ikiwa ni pamoja na vifaa vya ujenzi mpaka jengo hilo kufikia hatua ya boma.
Hata hivyo waziri Jafo amesema kuwa serikali itafanya jitihada za kuhakikisha ukamimilishaji wa jengo hilo unafanyika na kusisitiza kuwa mpaka kufikia mwezi Disemba,2018 jengo hili liwe limekamilika na wananchi waanze kupata huduma.
Ameongeza kuwa lengo la serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha kila kata inakuwa na kituo cha afya chenye hadhi ya nyota tano, chenye kulaza wagonjwa, jengo la kujifungulia, maabara, jengo la upasuaji na jengo la maiti 'mortuary' na vituo hivyo kuwa na dawa za kutosha.
Naye kaimu mkurugenzi halmashauri ya Arusha Paulus Kessy amesema kuwa, katika bajeti ya mwaka 2018/19, halmashauri imepanga bajeti ya shilingi milioni 10 kwa mwaka wa fedha 2018/19 kwa ajili ya uendelezaji wa miundombinu ya kituo hicho cha afya.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.