Na Elinipa Lupembe
Jamii imetakiwa kujifunza kutatua migogoro baina yao kwa njia mbadala, njia ambayo licha ya kuwa haina gharama kubwa, huleta amani kwa kupunguza uadui na kuondoa umasikini miongoni mwa wahusika ndani ya jamii.
Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, wakati akifungua Kampeni ya utoaji msaada wa Kisheria bure kwa wananchi, inayofanyika katika kata ya Ilkiding'a, halmasahuri ya Arusha, wilaya ya Arumeru.
Dkt. Ndumbaro amefafanua kuwa, Wizara yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, inao utaratibu wa kutoa msaada wa kisheria bure kwa wananchi, kwa kufanya usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala, lengo likiwa ni kuleta amani baina ya wahusika pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa kesi.
"Tunafahamu kuendesha kesi mahakamani kunahitaji gharama kubwa za kuweka mawakili, gharama ambazo wananchi wengi hushindwa kuzimudu na kukosa haki zao huku wakibaki na majeraha mioyoni mwao, kupitia kampeni hii, tunatoa msaada wa kisheria bure na kuhakikisha tunafanya usuluhishi kwa njia ya amani" Amefafanua Dkt Ndumbaro.
Aidha amebainisha kuwa utoaji wa huduma za kisheria bure, wizara yake inatekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020, ibara ya 120 kifungu D inayoelekeza kuimarisha mfumo wa usajili ili kutoa msaada wa kisheria bure, hususani kwa wananchi waiso na uwezo wa kumudu gharama za kuweka mawakili kusimamia kesi zao.
Naye Katibu Tawala mkoa wa Arusha, Missaile Musa, licha ya kuishukuru serikali kupitia wizara hiyo, amemuomba mheshimiwa Waziri, kampeni hiyo kufanyika katika wilaya zote za mkoa wa Arusha, kutokana na ukweli kwamba, mkoa huo unakabiliwa na migogoro mingi hususani ya ardhi na mipaka.
"Nikuombe mheshimiwa Waziri, kampeni hii isiishie hapa, ifanyike kwenye wilaya zote za mkoa wa Arusha, tuna uhitaji mkubwa wa msaada wa kisheria kwa wananchi wetu, wananchi wana migogoro ya ardhi na mipaka katika maeneo mengi, kupitia jukwaa hili, ninaamini migogoro mingi itatatuliwa na kurejesha amani miongoni na wananchi wetu".Amesisitiza Katibu Tawala huyo.
Hata hivyo Waziri Dkt. Ndumbaro, licha ya kukubali ombi hilo la Katibu Tawala, amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara yake, kuratibu jambo hilo katika mkoa wa Arusha na kwenda mbali zaidi kwa kufanya kampeni hiyo katika halmashauti zote nchini.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Arusha, Mheshimiwa Ojung'u Salekwa, amemuomba pia mheshimiwa Waziri, kupata wasaidizi wa Kisheria katika halmashauri hiyo, kwa kuwa ni huduma inayohitajika sana, kutokana na uwepo wa migogoro mingi na baadhi ya wananchi kupoteza haki zao kwa kushindwa kumudu gharama za uendeshaji wa kesi.
"Mheshimwa Waziri, wananchi wa halmashauri hii, wanakabiliwa na migogoro mingi ya kisheria ikiwemo migogoro ya ardhi na mipaka, kesi za ukatili na ubakaji, urithi na mirathi, ukandamizwaji wa wanawake na watoto, madhila ambayo kiuhalisia yanaondoa amani na utulivu miongoni mwa jamii, uwepo wa msaada wa kisheria bure, utatusaidia kutatua migogoro mingi" Amebainisha Mheshimiwa Mwenyekiti.
Awali, wananchi waliofika katika kampeni hiyo, wameipongeza Serikali na Wizara ya Sheria kwa kuona umuhimu wa kufanya kampeni hiyo, jambo ambalo licha ya kupata msaada lakini limewawezesha wananchi kujifunza mambo mengi juu ya upatikanaji wa haki zao kwa njia ya amani bila kuwa na migogoro wala uhasama miongoni mwao.
Jacob Lembris mkazi wa Sambasha, amesema kuwa kampeni hiyo imewafungua ufahamu wa namna bora ya utatuzi wa migogoro, usuluhishi nje ya mahakama, njia sahihi za kupata haki iliyopotea pamoja na kutambua umuhimu wa haki za watoto na wajibu wa wazazi kwa watoto wao.
Kampeni ya Kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi bure, yenye kauli mbiu ya "Utatuzi wa Migogoro kwa njia Mbadala, hupunguza Uadui na kuziua umaskini", inafanyika kwa siku mbili katika kata ya Ilkiding'a, ikijumuisha wakazi wa kata hiyo na kata za jirani za Sambasha, Olturoto na Kiranyi.
ARUSHA DC
TUPO KAZINI ✍✍✍
Waziri wa Sheria na Katiba, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, akizungumza na wanachi wa halmashauri ya Arusha wakati akifungua Kampeni ya Utoaji Msaada wa Kisheria bure, katika viwanja vya kanisa la KKKT kata ya Ilkiding'a.
Katibu Tawala mkoa wa Arusha, Massaile Musa, akizungumza mble ya mgeni rasmi na Waziri wa Sheria na Katiba , wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Utoaji Msaada wa Kisheria bure, katika viwanja vya kanisa la KKKT kata ya Ilkiding'a,.
Mwenyekiti halmashauri ya Arusha, Mhe. Ojung'u Sallekwa, akizungumza mble ya mgeni rasmi na Waziri wa Sheria na Katiba , wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Utoaji Msaada wa Kisheria bure, katika viwanja vya kanisa la KKKT kata ya Ilkiding'a.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.