Halmashauri ya Arusha imeadhimisha siku ya hedhi duniani huku jamii ikitakiwa kuvunja ukimya kwa kupaza sauti itakayoondoa usiri utakaomuwezesha mwanamke kuwa na mazingira bora yatakayomuwezesha kuwa hedhi salama.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika kwenye shule ya sekondari Mukulat, kata ya Lemanya na kushirikisha zaidi ya wanafunzi 500 kutoka shule tano za sekondari na shule mbili za msingi zilizo karibu na shule ya sekondari Mukulati.
Akizingumza wakati wa maadhisho hayo, Afisa Afya halmashauri ya Arusha, Issa Msumari amesema kuwa jamii inalazimika kuondokana na mila na desturi za usiri kuhusu hedhi na kuanza kuwa wazi ili kuweka mazingira salama ya kipindi chote atakapokuwa kwenye siku za hedhi.
Ameongeza kuwa wanawake wengi wamejikuta wakipata madhara ya kiafya, kisaikolojia na hata kiuchumi kutokana na hedhi isiyo salama inayotokana na usiri uliyopo ndani ya jamii.
Afisa Afya huyo ameyataja madhara yanayoweza kutokana na hedhi isiyo salama ni pamoja na maumivu makali, muwasho, michubuko, fungusi, maambukizi kwenye via vya uzazi pamoja na maambukizi kwenye njia ya mkojo UTI.
Hata hivyo amewataka wazazi na walezi, kuzungumza na watoto wa kike juu ya umuhimu wa hedhi salama bila kuona aibu sambamba na kuwawezesha kupata vifaa salama vya kujihifadhi wakati wakuwa kwenye hedhi.
Ni jukumu la jamii kuwawezesha wanawake hasa wasichana, kupata vifaa vya kutumia wakati wote wa hedhi, kuwa na utaratibu wa maeneo maalumu ya kujisitiri wakati wa kubadilisha vifaa namahali salama pa kutupa vifaa vilivyotunika, hii itamuwezesha mwanamke kuwa mkamilifu kipindi chote cha hedhi.
"Jamii inapaswa kutambua hedhi inahitaji rasilimali nyingi ikiwemo fedha ya kununua vifaa salama vya kujisitiri, inahitaji miundombinu mizuri ya kujihifadhi na kuanika vifaa visivyotumika mara moja, na inahitaji eneo la kuviteketeza baada ya kutumika, wanawake peke yao hawataweza" amesema Msumari
Aidha wanafunzi walioshiriki kwenye maadhimisho hayo, wamefurahia maadhimisho ya siku hiyo ya hedhi na kusema kuwa mafunzo waliyoyapata yamewawezesha kupata ujasiri na kujiamini siku zote za hedhi, tofauti na hapo awali walikuwa wanaona aibu, kuzungumzia suala zima la hedhi hata wakati mwingine mbele ya wasichana wenzao.
Mwanafunzi Judith Sikulumbwe amesema kuwa kupitia siku hiyo rasmi kwa wasichana na wanawake, amepata mwanga zaidi wa kuvunja ukimya na kuwa wazi pamoja na kutambua namna ya kujihifadhi, muda wa kuvaa vifaa hivyo, namn kuteketeza vifaa vilivyotumika, na kujihakikishia usafi binafsi.
Hata hivyo mwanafunzi, Pendo Frank amesema kuwa amefurahia elimu waliyoipata na itawasaidia kuanzisha klabu kwenye shule zao, ambazo zitawafanya kuwa huru kujadili masuala ya hedhi salama na kuwafundisha wenzao kwa kushirikushana na walimu na walezi wa shule 'matron'.
Naye mratibu wa miradi, shirika la WaterAid Tanzaniam Upendo Muntambo amesema kuwa, ingawa mila na desturi zinafanya hedhi kuwa siri na kupelekea msichana kuwa na wigo awapo kwenye siku zake, mila hizo zisizuie wasichana na wanawake kujihakikishia hedhi salama yenye kumfanya mwanamke kuwa mwenye furaha wakati wote wa siku zake za hedhi.
Gudila Joakim mdau kutoka shirika la AceAfrica amefafanua kuwa, hedhi ni kitu cha kujivunia kwa mwanamke na huthibitisha kuwa mwanamkr aliyekamilika, na kutoa wito kwa watoto wa kiume kushirikiana vyema na watoto wa kike na sio kuwatenga pindi wanapopatwa na hali hiyo.
Maadhimisho ya siku ya hedhi yanafanyika kila tarehe 28.05 kila mwaka na mwaka huu yakiwa na kauli mbiu ya 'HAKUNA TENA KIKWAZO' yenye lengo la kuifanya jamii kushirikiana na kuhakikisha wanawake wanapata hedhi salama itakayomuwezesha kujisikia huru, mwenye furaha na mwenye kutekeleza majukumu yake bila kikwazo.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.