Na. Elinipa Lupembe.
Halmashauri ya Arusha, wilaya ya Arumeru, imeanza rasmi mchakato wa kuweka sawa mazingira ya shule zake tayari kwa kukabiliana na kujikinga na gonjwa hatari la Corona, kwa kuanza kweka vifaa vya kunawia mokono katika shule zote za sekondari na msingi za halmashauri hiyo.
Imeelezwa kuwa, maandalizi hayo yameanza rasmi, kufuatia agizo la mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, kutangaza kuwa maambukizi ya ugonjwawa Corona yamepungua nchini na kuwataka wananchi kuendelea kufanyakazi huku wakijikinga na ugonjwa huo, kwa kuwa licha ya ugonjwa huo kuwepo, maisha nayo lazima yaendelee.
Afisa Elimu Msingi, halmashauri ya Arusha, Hossein Mghewa, amekabidhi jumla ya ndoo 295 za kunawia mikono kwenye shule za serikali 95 za halmashauri hiyo na kuwataka walimu wakuu wa shule hizo, kufanya maandalizi ya kuhakikisha wanafunzi watasoma kwenye mazingira bora bila kupata maambukizi ya ugonjwa huo wa Corona pindi serikali itakapotangaza kufungua shule hizo.
Mghewa ameeleza kuwa vifaa hiviyo ni maandalizi, pindi serikali itakapotangaza shule kufunguliwa, kwa ajili ya kudhibiti na kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa Corona unaosababishwa na Virusi vya Covid 19, na kuwataka walimu kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika ipasavyo kwa kufuata maelekezo ya watalamu wa afya.
"Tumejipanga kukabiliana na ugonjwa wa Corona kwa kuhakikisha kila shule ina vifaa vya kunawia mikono, maji safi yanayotiririka na sabuni, ili wanafunzi waweze kunawa mikono mara kwa mara chini ya usimamizi wa walimu wao" amesema Afisa Elimu huyo.
Nao walimu wakuu licha ya kuishukuru serikali kwa kutoa vifaa hivyo shuleni, wameahidi kusimamia vema suala zima la kujikinga na ugonjwa wa Corona, kwa kusimamia ipasavyo maelekezo yote yanayotolewa na watalamu wa Afya na kuwaelekeza wanafunzi kufuata tabia chanya za usafi wao binafsi.
Katibu wa Walimu Wakuu na Mwalimu Mkuu shule ya Msingi Emaoi, amesema kuwa, walimu wanapaswa kujiandaa kisaikolojia kuwa, wanakazi ya ziada ya kuhakikisha wanafunzi wanafuata taratibu zote za kujikinga na ugonjwa wa Corona, kwa kuwadhibiti watoto kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni pindi shule zitakapokuwa zimefunguliwa.
"Ugonjwa upo, lazima tukabiliane nao, tunatakiwa kuwafundisha watoto namna ya kujikinga na maambukizi ya Corona, kwa nadharia na vitendo huku masomo yakiendelea" amesema Katibu huyo.
Halmashauri ya Arusha inaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo, kupambana na ugonjwa wa Corona, ugonjwa ambao hauna kinga wala tiba na umeenea kwa kasi duniani kote.
Afisa Elimu Msingi halmashauri ya Arusha, akimkabdhi ndoo za kunawia mikono1 Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Ngaramtoni, mwalimu Makanjo Twati tayari kwa maandalizi ya kukabiliana na ugonjwa wa Corona pindi shule zitakapofunguliwa.
Baadhi ya Walimu Wakuu shule za Msingi, halmashauri ya Arusha wakiwa na ndoo za kunawia mikono kwa ajili ya shule zao, tayari kwa maandalizi ya kukabiliana na ugonjwa wa Corona pindi shule zitakapofunguliwa.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.