Na. Elinipa Lupembe
Halmashauri ya wilaya ya Arusha imeendelea kuridhishwa na huduma zinazotolewa na wadau wa elimu wa shirika lisilo la kiserikali la A FOR AFRICA, na kuamua kuwapatia cheti cha utambuzi, kutokana na jitihada za utendaji kazi na huduma zinazoendelea kuonekana na kuzaa matunda huku juhudi hizo zikiiendeleza sekta ya elimu katika halmashauri hiyo.
Akikabidhi cheti hicho, alipokutana na wadau wa shirika hilo, ofisini kwake, mapema wiki hii, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Dkt. Wilson Mahera alipata wasaa wa kufanya mazungumzo marefu na kumkabidhi cheti hicho mmoja wa waanzilishi na mwakilishi wa tasisi ya A IS FOR AFRICA Bi. Mariane RickSmith, na kusema kuwa cheti hicho, ni ishara ya kushukuru na kuthamini, mchango mkubwa unaotolewa na shirika hilo kwa kipindi kirefu sasa katika halmashauri yake.
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa, halmashauri imefurahishwa na kuridhishwa na jitihada zinazofanywa na shirika hilo, kwa kusaidia uetekelezaji wa shughuli za elimu unaosaidia urahisi wa kufundisha na kujifunza kwa walimu na wanafunzi wa shule ya msingi Matimu kata ya Lemanyata.
Aidha Dkt. Mahera amefafanua kuwa shirika hilo limekua likiisaidia shule hiyo ya Msingi Matimu, kwa kipindi cha miaka kumi sasa, na kuzitaja huduma zinazotolewa na shirika hilo ni pamoja uanzishwaji wa darasa la kompyuta lenye jumla ya kompyuta 35 zilizounganishwa na mfumo wa intaneti.
Wadau hao pia wamekua wakitoa uji kwa wanafunzi wote shuleni hapo, kwa kipindi chote cha mwaka, pamoja na kuwapatia walimu wote chai na chakula cha mchana, jambo ambalo linasaidia walimu na wanafunzi kuwa na furaha wakati wote wa masomo, wawapo shuleni.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo, ameahidi kuendelea kushirikiana na wadau wa shirika hilo, katika kutekeleza adhma ya Serikali ya awamu ya tano, ya kuhakikisha, shule zote zinakuwa na miundombinu bora na rafiki kwa wanafunzi na walimu, huku akiwataka wadau wengine kujitokeza kusaidia utekelezaji wa adhma hiyo ya serikali.
“Kama halmashauri tuko tayari kutoa ushirikiano, kwa wadau binafsi na mashirika wanaofanya kazi na kutoa huduma ndani ya halmashauri yetu katika sekta zote, lengo likiwa ni kusukuma mbele gurudumu la maendeleo na kujenga ustawi wa jamii na taifa letu." Amesema mkurugenzi huyo.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa cheti hicho, mwakilishi wa shirika la A FOR AFRICA, Bi. Maryanne Rick, amesema kuwa, lengo la msaada huo ni kuunga mkono juhudi za serikali ya Tanzania kwa kuwawezesha watoto wa kitanzania ni kuweza kuendana na dunia ya Sayansi na teknolojia kwa kujifunza kutumia kompyuta kuanzia shule ya msingi.
" Ni vema mtoto akaandaliwa kutumia kompyuta kuanzia akiwa na umri mdogo, hii itamjengea kujiamini kupenda kujifunza zaidi, hata atakapofikia kwenye elimu ya sekondari, elimu ya juu hata awapo katika kazi" amethibitisha Bi. Maryanne
Hata hivyo Bi. Maryanne amesema kuwa kwa sasa shirika limepanua wigo wa kutoa msaada na kuweza kusadia pia shule jirani ya sekondari Makulat, kwa kufanya marekebisho kwenye vyumba kumi vya madarasa, kufanya marekebisho kwenye maktaba ya shule hiyo kwa kuongeza vitabu vya kiada na ziada.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule ya msingi Matimu, mwalimu Ang’weni Lang’o licha ya kulishukuru shirika hilo, amesema kuwa maabara hiyo ya kompyuta, inawasaidia sana wanafunzi kujifunza matumizi ya kompyuta pamoja na waalimu kutumia kuandalia mitihani, jambo linalosaidia kupunguza gharama za maandalizi ya mitihani zilizokuwa zikitumika hapo awali.
Ameongeza kuwa, pamoja na kompyuta hizo kutumika kama nyenzo za kujifunzia na kufundishia lakini pia zimewaongezea wanafunzi wake ari ya kupenda shule, na zaidi kwa kupandisha mahudhurio huku utoro wa wanafunzi shuleni ukipungua kwa kiasi kikubwa.
Halmashauri ya Arusha, inatoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia, uwezeshaji wa mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia katika shule zake za msingi na sekondari.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.