Na Elinipa Lupembe
Halmashauri ya Arusha imevuka lengo lililotarajiwa katika Kampeni ya Chanjo ya Polio awamu ya tatu, kwa kutoa chanjo ya Polio kwa jumla ya watoto 96,296 kati ya watoto 88, 628 wa chini ya miaka mitano, sawa na asilimia 108.6.
Akizungumza Ofisini kwakwe na mwandishi habari hizi, Mganga Mkuu halmashauri ya Arusha, Dkt. Petro Mboya amethibitisha kuwa, idadi ya watoto waliopatiwa chanjo ya Polio wakati wa Kampeni ya chanjo hiyo kwa awamu ya 3, imezidi makisio na kufikia asilimia 108.6.
Daktari Mboya ametaja siri kubwa ya mafanikio ya kuvuka malengo ni kutoa elimu na hamasa kwa jamii juu ya umuhimu wa chanjo hiyo, pamoja na mikakati thabiti kwa kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii, iliyowawezesha kutoa huduma hiyo nyumba kwa nyumba.
"Makadirio yalikuwa ni kuchanja watoto 88, 628 lakini tumefanikiwa kuchanja watoto 96, 298, ninawapongeza wazazi na walezi kwa kuhakikisha watoto wao wamepata chanjo, zaidi ninaipongeza Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Arumeru ikiongozwa na Mhandisi Ruyango kwa ushauri na usimamizi pamoja na timu nzima ya afya halmashauri ya Arusha". Amesisitiza Dkt. Mboya.
Ikumbukwe kiwa, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Chanjo ya Polio awamu ya 3, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhandisi Richard Ruyango, alisistiza kuhakikisha watoto wote wamepata chanjo ya Polio ili kudhibiti ulemavu pamoja na vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Polio kwa kuwa kuna chanjo ya kutosha.
Naye mratibu wa Chanjo, halmashauri ya Arusha, Muruta Kiboko, amewasisitiza wazazi na walezi wenye watoto ambao, hawajamaliza chanjo za Polio kuendelea kuwapeleka watoto kliniki kupata chanjo hizo licha ya kuwa wamechanjwa kupitia kampeni hiyo iliyofanyika kwa siku 4.
Awali Kampeni ya Chanjo ya Polio yenye kauli mbiu ya Mpe chanjo,Okoa Maisha, imetekelezwa nchini na Serikali kwa kushirikiana na wafadhili wa shirika la Watoto UNICEF pamoja na shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lengo likiwa kuwakinga maisha ya watoto.
Mpe Matone..., Okoa Maisha
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.