Benki ya Posta Tanzania - TPB, imejipanga kupandisha kiwango cha taaluma kwa wasichana wanaosoma, shule ya sekondari Nduruma, halmashauri ya Arusha, wilayani Arumeru.
Mkakati huo umewekwa wazi na Afisa Mtendaji Mkuu Benki ya Posta Tanzania, Sabasaba Moshingi, wakati wa hafla fupi ya kukabidhi msaada wa matofali 1000 na mifuko 100 ya saruji, vyenye tamani ya shilingi milioni 3.5, kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa bweni la wasichana, iliyofanyika shuleni hapo mwishoni mwa wiki iliyopita.
Moshingi amesema kuwa, Benki ya Posta Tanzania, imeamua kutoa msaada huo, kwa lengo la kuwanusuru wasichana wa shule ya sekondari Nduruma, kutoka na changamoto wanazokumbana nazo, kuanzia nyumbani mpaka kufika shuleni, zinazochangia kushindwa kufanya vizuri kwenye masomo yao, pamoja na kuunga mkono juhudi za wananchi wa Nduruma, ambao tayari wamekamilisha ujenzi wa msingi wa jengo la bweni hilo.
Ameongeza kuwa, licha ya kuwa watoto wote kuwa na haki sawa, lakini watoto wa kike wapo kwenye hatari kubwa wakiwa njiani kuelekea shuleni, hatari zinayowasababishia mimba na ndoa za utotoni hadi kufikia kushindwa kuendelea na masomo na kukatiza ndoto zao.
Aidhaa Moshingi, amefafanua kuwa, Benki ya Posta Tanzania, ni benki ya watanzania hivyo, hutoa kiasi cha faida inayoipatikana na kuirudusha kwenye jamii, kwa kuchangia miradi mbalimbali kwenye sekta za elimu na afya, sambamba na kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha miundombinu kwenye sekta hizo, ili wananchi waweze kupata huduma bora zaidi.
Naye Mkuu wa shule ya sekondari Nduruma mwalimu, Hilda Zoya licha ya kuishukuru Benki hiyo ya Posta, amethibitisha uwepo wa changamoto ya umbali wa maeneo, wanayoishi wanafunzi wa shule hiyo, jambo linalosababisha kushindwa kufanya vizuri kwenye masomo yao, huku kiwango cha ufaulu kikiwa ni cha chini.
Ameeleza kuwa, wanafunzi wa shule hiyo, wametoka kwenye jamii ya wafugaji, jamji ambayo wengi huishi mbali kutafuta malisho, na kuwafanya baadhi ya wanafunzi kutembea kati ya Kilomita kumi na kumi na tano, kwenda na kurudi shuleni kila siku, na kuwasababishia uchovu na wengine kushindwa kuhudhuria shuleni kila siku, jambo linaloathiri kwa kiasi kikubwa mchakato mzima wa kufundisha na kujifunza.
"Wanafunzi wakifika shuleni wamechoka na wakati mwingine mahudhurio yao ni ya kususua na kusababisha ufundishaji kuwa mgumu, pamoja na kudumaza taaluma na ufaulu kuwa wa kiwango cha chini" amesema mkuu huyo wa shule.
Hata hivyo wanafunzi wa shule hiyo, wameishukuru benki hiyo, kwa kutambua changamoto yao, na kueleza kuwa uwepo wa mabweni hayo ya wasichana, utaongeza ari ya kusoma na kupenda shule, ari ambayo inatoweshwa na umbali mrefu wanaotembea wakati wa kwenda na kurudi shuleni na kusababisha uchovu na kukata tamaa.
Eliya Obadia, mwanafunzi wa kidato cha tatu, amefafanua kuwa, wasichana ndio wanaoathirika zaidi na changamoto ya umbali huo, hasa wakati wa mvua, hushindwa kuvuka makorongo yaliyojaa maji na kushindwa kuhudhuria shuleni pindi mvua kubwa zikinyesha.
"Wakati wa mvua makorongo hujaa maji, wasichana wanogopa kuvuka, bora sisi wavulana huwa tunajitahidi kupambana kuvuka lakini mara nyingi wasichana wao hushindwa na kulazimika kurudi nyumbani" amethibitisha Eliya.
Mwenyekiti wa Kamati ya shule, Thobias Lonyamali, amewataka wanafunzi hao, kuongeza bidii katika masomo yao na kutambua kuwa, wazazi wao wanajinyima mahitaji mengine na kuamua kuchangia ujenzi wa miundombinu ya shule, ili wao waweze kusoma vizuri kwa mafamikio yao ya baadaye.
Awali ujenzi wa bweni hilo unategemea kugharimu kiasi cha shilingi milioni 56 na mpaka sasa msingi wa bweni hilo, umekamilika kwa kujengwa kwa nguvu za wananchi wa kata ya Nduruma kwa gharama ya shilingi milioni 5.2, huku bweni hilo likitegemewa kulaza jumla ya wanafunzi wakike 70.
Shule ya sekondari Nduruma ina jumla ya wanafunzi 544, ikiwemmo wavulana 234 na wasichana 310, ikiwa inakabiliwa na changamoto ya wanafunzi kuishi maeneo ya mbali na shule, changamoto inayosababisha wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni.
PICHA ZA MATUKIO:
Afisa Mtendaji Mkuu Benki ya Posta Tanzania, akimkabidhi mifuko ya saruji, mkuu wa shule ya sekondari Nduruma mwalimu Hilda Zoya.
Afisa Mtendaji Mkuu, Benki ya Posta Tanzania, akikabidhi matofali wa Mkuu wa shule ya sekondari Nduruma, mwl. Hilda Zoya(katikati) na Afisa Elimu Taaluma Idara ya Elimu Sekondari Charles John (wa kwanza kulia)
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.