CRDB YAAZIMISHA MIAKA 30 KWA KUGUSA MAISHA: YAKABIDHI DARAJA LA ELIMU KWA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI
Katika kuadhimisha miaka 30 ya huduma na mchango wa maendeleo kwa jamii, Benki ya CRDB imekabidhi darasa, madawati, magodoro, na televisheni kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Emaoi, iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.
Msaada huu umetolewa kwa niaba ya Benki na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Prof. Faustine Bee, na kukabidhiwa rasmi kwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Amir Mohammed Mkalipa, kama ishara ya ushirikiano wa karibu kati ya Benki ya CRDB na Jamii katika kuendeleza sekta ya elimu nchini.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Prof. Bee alieleza kuwa Benki ya CRDB hutenga asilimia moja ya faida kabla ya kodi kila mwaka kupitia Sera yake ya Uwekezaji kwa Jamii, ili kusaidia sekta za elimu, afya, na mazingira.
Prof.Bee aliongeza kwa kusema kuwa CRDB kupitia kampeni zake kama vile Keti Jifunze na Pendezesha Tanzania, Benki hiyo imekuwa mshirika thabiti wa Jamii kupitia Serikali katika kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata mazingira bora ya kusima na kujifunzia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Amir Mkalipa aliipongeza Benki ya CRDB kwa mchango mkubwa wanautoa katika Jamii, akitolea mfano wa ujenzi wa darasa pamoja na utoaji wa vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na kusema kuwa hatua hiyo ni ya muhimu katika kuinua elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum.
" kwa kweli Msaada huo ni sehemu ya shughuli za kijamii zinazotekelezwa kuelekea Mkutano wa 30 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB, unaotarajiwa kufanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 16,Mei,2025 na kufunguliwa na Makamu wa Rais Dkt.Philip Isdor Mpango,,hivyo sisi kama Serikali tunaishukuru Benki ya CRDB kwa mchango wake kwa Jamii".Alisema Mkalipa.
Benki ya CRDB inaamini kuwa msaada huu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum utawapa fursa ya elimu bora na maisha yenye mafanikio. Katika kuadhimisha miaka 30 ya huduma, Benki imeahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali na wadau mbalimbali ili kuleta maendeleo ya kweli na yenye kuwagusa wananchi moja kwa moja.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.