Na Elinipa Lupembe
Kufuatia mkakati wa Serikali wa kutokomeza ugonjwa wa Polio nchini, wilaya ya Arumeru yenye halmashauri za Arusha na Meru, inatekeleza mkakati huo kwa kutoa chanjo ya Polio kwa watoto wa chini ya miaka 5, huku Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Mhandisi Richard Ruyango akisisitiza, kuwa hakuna mtoto wa Arumeru atapooza kutokana na ugonjwa huo wa Polio.
Mkuu huyo wa wilaya amebainisha hilo, wakati akizindua kampeni ya chanjo ya Polio awamu ya tatu, inayohusisha watoto wa kuanzia umri wa miaka 0 - 5, uzinduzi uliofanyika katika Zahanati ya Lengijave halmashauri ya Arusha.
Mhandisi Ruyango amethibitisha kuwa halmashauri zote za wilaya ya Arumeru, zimefanya vizuri katika kuhakikisha watoto wa chini ya miaka 5, wamepata chanjo kwa awamu ya kwanza na ya pili, huku awamu hii ya tatu, wakiwa wamejipanga kufikia malengo waliyojiwekea ya kufikia watoto 145,219.
"Tumejipanga vema kuhakikisha tunawafikia watoto wote wa chini ya miaka mitano na kuhakikisha wanapata chanjo ya Polio, lengo letu ni kuhakikisha hakuna mtoto wa Arumeru atapooza kwa ugonjwa huo, kwa kuwa mkakati wetu ni kuwapa chanjo watoto". Amesisitiza Mkuu huyo wa wilaya
Hata hivyo, uzinduzi huo ulipambwa na wanaume kuwaleta watoto kuoata chanjo, wakiwa kifua mbele kuhamasisha wanaume wenzao kushirikiana na wenza wao kuhudhuria Kliniki wakati wote wa ujauzito na watoto wa chini ya miaka mitano.
Joshua Samweli (28) baba wa mtoto Prisca Joshua mwenye umri wa mwezi (1), amesema kuwa yeye huudhuria Kliniki na mwenza wake tangu wakati wote wa ujauzito, lengo lake ni kufahamu maendeleo ya makuzi ya mtoto wake tangu akiwa tumboni, kuzaliwa mpaka kukua kwake.
Naye Julius Mathayo baba wa mtoto Gloria Losieku (1), amesema kuwa amelazimika kumpeleka mtoto wake kupata chanjo, ili kumkinga na ugonjwa wa Polio unaosababisha ulemavu wa kudumu na wakati mwingine kifo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi, amethibitisha kutimiza maagizo ya mkuu wa wilaya kwa kuhakikisha watoto wote wanapatiwa chanjo ya Polio na kuongeza kuwa, halmashauri imejipanga kwa kuwa na vituo 59 vya kudumu vya kutolea huduma za Afya pamoja na pamoja na posti 201 zilizoandaliwa kwa ajili ya kutoa chanjo hizo wakati huu wa kampeni, kwenye ofisi za kata, vijiji na vitongoji.
Mganga mkuu halmashauri wa Arusha, Dkt. Petro Mboya, amekiri kuhakikisha wanadhibiti ugonjwa wa Polio kwa kuhakikisha watoto wote wanapata chanjo zote dhidi ya ugonjwa wa Polio mara baada ya kuzaliwa na kukamilisha chanjo zote.
Aidha ameweka wazi kuwa, katika Kampeni ya Chanjo awamu ya (3), halmashauri hiyo inategemea kutoa chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Polio kwa watoto 88,628.
Ikumbukwe kuwa Kampeni ya Chanjo ya Polio yenye kauli mbiu ya Mpe chanjo, Okoa Maisha, inatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wafadhili wa shirika la Watoto UNICEF pamoja na shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lengo likiwa kuokoa maisha ya watoto.
Mpe Matone........, Okoa Maisha
ARUSHA DC
TUKO KAZINI✍
HAKIKISHA UMEHESABIWA
PICHA ZA MATUKIO WAKATI WA ZOEZI LA UZINDUZI WA KAMPENI YA CHANJO AWAMU YA 3 ZAHANATI YA LENGIJAVE
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhandisi Richard Ruyango akimpatia mtoto Veronica Meru (miezi 3) matone ya chanjo ya Polio, ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa Kampeni ya chanjo ya Polio awamu 3, halmashauri ya Arusha kwenye Zahanati ya Lengijave
Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi, akimpatia mtoto Gloria Losieku (1) matone ya chanjo ya Polio, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya chanjo ya Polio awamu 3, kwenye Zahanati ya Lengijave
Mganga mkuu halmashauri ya Arusha, Dkt. Petro Mboya, akimpatia mtoto Prisca Joshua (Miezi 3) matone ya chanjo ya Polio, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya chanjo ya Polio awamu 3, kwenye Zahanati ya Lengijave
Wauguzi Halmashauri ya Arusha wakifurahia kumhudumia baba Julius Mathayo aliyeleta mtoto wake kupata chanjo ya Polio kwenye Zahanati ya Lengijave wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya chanjo ya Polio awamu 3,
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.