Na. Elinipa Lupembe.
Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika 2022, mkoa wa Arusha, umejipanga kuendelea kupambana na ukatili dhidi ya watoto kwa kuwataka wazazi na walezi kuacha kukwepa majukumu yao ya malezi kwa watoto wao, jambo ambalo linasababisha watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili ndani ya familia zao.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo ya siku moja, yaliyojumuisha waandishi wa habari, watoto, watalam na wadau, Katibu Tawala mkoa wa Arusha, Dkt. Athman Kihamia, ameweka wazi kuwa mkoa wa Arusha, umeweka mikakati ikiwemo kuelekeza nguvu katika kuimarisha juhudi za kumlinda mtoto wa mkoa wa Arusha dhidi ya ukatili na hatimaye kutokomeza ukatili mkoani humo huku akiwataka wazazi kuwa karibu na watoto wao, licha ya changamoto za utafutaji wa riziki na vipato vya familia.
Licha ya kuwa serikali ina mikakati imara ya kupambana na ukatili dhidi ya watoto, zaidi amewataka wazazi na walezi kutekeleza majukumu yao ya malezi kwa kuwasimamia watoto na si kuwaachia walimu ama wasaidizi wao wa nyumbani, kulea watoto wao, jambo ambalo limekuwa ni sababu ya watoto wengi kufanyiwa ukatili bila wazazi kufahamu kwa kuwa wanawaamini watu hao.
Amefafanua kuwa jukumu la malezi ya watoto ni wazazi, lakini wazazi wamejikita zaidi kufanya kazi kwa ajili ya kujipatia kipato na kuacha jukumu la malezi kwa walimu na wasaidizi wa ndani jambo ambalo linasababisha watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili ndani ya nyumba zao.
"Matukio mengi ya ukatili yanafanyika ndani ya familia zetu na ndugu wa karibu tunaowaamini, kama wazazi watatimiza wajibu wao wa kulea watoto, watoto watakuwa katika maadili mema na matukio ya ukatili yatapungua, na hatimaye kuwa na jamii yenye maadili mema, lakini wazazi wamekuwa chanzo cha watoto kufanyiwa ukatili majumbani" amesisitiza Katibu Tawala huyo.
Naye Inspekta Happy Mshana, kutoka Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha, amekiri kuwepo na uzembe mkubwa unaofanya na wazazi katika malezi ya watoto, kwani asilimia kubwa ya wazazi hawawafamu vizuri watoto wao, kutokana na muda mwingi kuwaachia walimu, wasaidizi wa kazi ama ndugu wanaoishi nao nyumbani, miongoni mwao ndio wanawafanyia watoto ukatili huku akiwalaumu baadhi ya wazazi kuwasaidia wahalifu wa ukatili kutoroka kwa kufanya nao maridhiano nyumbani.
"Katika kesi za watoto tunazozipokea, wazazi wengi hawajui tabia za watoto wao, kutokana na ubizy wa kuoambana na maisha, ukikaa na watoto wanaeleza mambo ambayo hata wazazi wao hawayajui, na ukiwapeleleza kwa undani, wanasema sisi tunabaki na dada, anko au mamdogo, jambo ambalo linatoa mwanya kwa watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili, niwatake wazazi kuwa karibu na watoto wao, ili kuwajua vema na kufahamu changamoto zizowakabili" amesisitiza Inspekta Happy.
Hata hivyo, watoto kutoka shule za tofauti za mkoa wa Arusha, wameishukuru serikali kupitia wimbo maalumu kwa kuanzisha Dawati la Jinsia na Watoto, Dawati ambalo limewezesha kutatua changamoto za watoto wanaofanyiwa ukatili, huku baadhi ya watoto wakipata wakipata haki zao, na watuhumiwa kuhukumiwa kutokana na makosa yao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, kupitia kitengo cha Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na wadau wa shirika la DSW, CWCD na SOS Children Village, wameandaa, mafunzi ya siku moja yaliyojumuisha waandishi wa habari, watalamu, watoto na wadau, ikiwa ni maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yenye kauli mbiu "Tuimarishe ulinzi wa mtoto; Tokomeza Ukatili Dhidi yake: Jiandae Kuhesabiwa"
#KaziIendelee✍✍
PICHA ZA MATUKIO WAKATI WA MAFUNZO
Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Dkt. Athman Kihamia, akizungumza wakati wa kufungua mafunzo juu ya mapambano ukatili dhidi ya watoto, mafunzo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano, ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arusha.
Watoto wakifuatilia mada zilizokuwa zinatolewa wakati wa mafunzi ya mapambano ya ukatili dhisi ya watoto, kwenye ukumbi wa Ofisi ya MKuu wa mkoa wa Arusha.
Inspekta Happy Mshana, kutoka Dawati la Jinsia na Watoto, mkoa wa Arusha, akifuatilia mada zilizotolewa juu ya mapambano ya ukatili dhidi ya watoto, kwenye ukumbi wa mikutano, ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arusha.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.