Halmashauri ya Wilaya ya Arusha yatoa Mafunzo Kwa Watendaji wa Kata na Vijiji kupitia mfumo wa TAUSI ili kuboresha utoaji wa huduma ya ukusanyaji wa kodi za majengo,mabango na utoaji wa vibali vya ujenzi kidigitali na kupunguza usumbufu kwa wananchi kufika Halmashauri kwa ajili ya kupata huduma hizo.
Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo bwana Seleman Msumi amesema kuwa, awali huduma ya ukusanyaji wa kodi za majengo na mabango zilikuwa zikitolewa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa njia ya analogia na kwa sasa huduma hizo zimerejeshwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI na zitakuwa zikikusanywa na Watendaji wa Mitaa badala ya kuajiri watu wa kukusanya huku vibali vya ujenzi vitakuwa vikitolewa na wataalamu kidigitali pasipo mwananchi kulazimika kufika ofisini.
Msumi mesema kuwa, kupitia mfumo wa TAUSI mwananchi anaweza kupata kibali cha ujenzi ndani ya siku moja tofauti na awali ambapo vibali vilikuwa vikichukua muda mrefu na kuwafanya wananchi kupata usumbufu wa ufuatiliaji usiokuwa na lazima.
Pia, amesema kuwa kutokana na baadhi ya majengo kutolipiwa kodi ya majengo kwa kukosa umeme kupitia mfumo wa TAUSI majengo yote yanayotumika wamiliki watatakiwa kulipa kodi baada ya watendaji wa Kata, Vijiji na Vitongoji kuwasajili kwenye mfumo huo.
Kwa upande wake Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha CPA Shabani Kisija amebainisha kuwa kupitia ukusanyaji wa kodi hizo Halmashauri kupitia makusanyo ya kodi za majengo itapata asilimia 20 na asilimia 100 kupitia makusanyo ya ushuru wa mabango ambapo awali fedha hizo zilielekezwa Serikali kuu.
CPA Shabani metoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Watendaji watakapokuwa wakipita katika maeneo yao kwa ajili ya usajili kwani kodi hizo sio mpya bali ni maboresho yaliyofanyika kutoka analogia kwenda digitali ili kurahisisha utoaji na upatikanaji wa huduma kwa ufanisi.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.