Zaidi ya shilingi milioni 296.4 za TASAF zimeanza kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu kwenye sekta ya Elimu na Afya katika kata za Bangata, Sambasha na Bwani, halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru.
Miradi hiyo kwa pamoja, inategemea kukamilika katika mwaka huu wa fedha wa 2018/19 na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa maeneo hayo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mratibu wa TASAF wa halmashauri ya Arusha, Grace Makema, amesema kuwa, kiasi hicho cha fedha kinatumika kutekeleza jumla ya miradi minne katika sekta ya elimu na afya.
Amefafanua kuwa katika miradi ya elimu jumla ya shilingi milioni 194.4 zimetumika kwenye ujenzi wa nyumba mbili za walimu zenye sehemu mbili (2in 1) katika shule ya msingi Mungushi kata ya Bwawani, ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa, ofisi ya walimu na vyoo shule ya sekondari Sambasha pamoja ujenzi wa nyumba ya walimu shule ya msingi Engikaret kata ya Bangata.
Aidha ameitaja gharama za kila mradi na kufafanua kuwa, ujenzi wa vyumba vya madarasa na choo chenye matundu sita, shule ya Sekondari Sambasha umegharimu kiasi cha shilingi milioni 74.3, na nyumba ya walimu Engikarate shilingi milioni 50 na nyumba ya walimu shule msingi Mungushi umegharimu kiasi cha shilingi milioni 70.
Makema ameutaja mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Midawe katika kata ya Bangata, mradi unaogarimu zaidi ya shilingi milioni 102.
Hata hivyo Mratibu huyo, amethibitisha kuwa, chanzo cha miradi hiyo ni wananchi wa maeneo husika ambao waliibua miradi hiyo kutokana na vipaumbele vyao na baadaye kupitishwa kwenye mikutano mikuu ya vijiji kwa makubaliano ya wananchi, ambayo ilifanyika katika mwaka wa fedha 2016/2017 na ikaanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha wa 2017/2018.
Pia amebainisha kuwa lengo la TASAF kutekeleza miradi hiyo ni kuwapunguzia wananchi mzigo wa kuchangia fedha kwaajili ya kugharamia ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za jamii pamoja na kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.
“ TASAF iliamua kutekeleza miradi hiyo yote katika maeneo hayo baada ya kuthibitisha kuwa kuna uhitaji wa miradi hiyo kutekelezwa katika maeneo hayo, ili kuwawezssha wananchi kupata huduma kwa urahisi" amesema Mratibu huyo
Kwa upande wake, mjumbe wa serikali ya kijiji cha Sambasha, Samweli Kwesam, ameishukuru serikali kupitia miradi yake ya TASAF kwa kutekeleza mradi wa madarasa na vyoo katika shule ya sambasha, ambao kwa kiasi kikubwa umewasaidia wananchi kuepuka kuchangia garama kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo.
Aidha amesema kuwa, shule hiyo ilikuwa na uhaba mkubwa wa vyumba vya madarasa kutokana na shule hiyo kuwa ni changa na wananchi walianza kuchangishana na kujenga chumba kimoja cha darasa lakini kutokana na juhudi za serikali, hadi sasa shule hiyo ina jumla ya vyumba kumi vya madarasa ambayo mawili kati ya hayo yamejengwa na TASAF na kutosheleza wanafunzi wote..
“Kama wananchi wa Sambasha, tuliithamini elimu na mwaka 2014 wananchi tulishirikiana na viongozi wetu na kuamua kujenga, jengo moja ambalo mwaka 2015 wanafunzi walianza kusoma lakini mpaka sasa hivi tuna majengo kumi pamoja na maabara tatu za kisasa”alisema Kwesam.
TASAF awamu ya III inatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo, miradi ya ujenzi, miradi ya mazingira, mifugo, kilimo pamoja na mradi wa uhawilishaji fedha kwa kaya masikini.
Vyumba vya madarasa na ofisi ya walimu, shule ya sekondari Sambasha kata ya sambasha.
Nyumba ya walimu yenye sehemu mbili (2 in 1)shule ya msingi Mungushi kata ya Bwawani.
Nyumba ya walimu yenye sehemu mbili (2 in 1) shule ya Msingi Engikaret kata ya Bangata.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.