Na Elinipa Lupembe
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha ndugu Steven Zelothe Steven na familia yake, tayari ametimiza wajibu wake, kama Mkuu wa Kaya, kwa kuhesabiwa kwenye Sensa ya Watu na Makazi nyumbani kwake eneo kitongoji cha Olosiva kata ya Oloirieni mapema leo.
Mwenyekiti Zelothe, akiwa na mkewe mama Janeth Zelothe, ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa, mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, zoezi ambalo linatarajiwa kuwa na matokeo chanya na makubwa ya kimaendeleo nchini.
Amefafanua kuwa licha ya kuwa zoezi la Sensa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020 -25, lakini pia, ni zoezi lenye mafanikio makubwa kwa maendeleo ya watanzania kwa kuiwezesha serikali kupanga mipango ya kimaendeleo kisekta kwa kuzingatia idadi ya watu kwa makundi yao.
Aidha amekiri kushiriki zoezi la Sensa mara kadhaa na kuweka wazi kuwa Sensa ya mwaka huu ni tofauti na Sensa zilizopita, Sensa iliyoandaliwa kukusanya takwimu kupitia mfumo wa kidigitali, jambo ambalo linatoa taswira ya kuwa na takwimu nyingi zilizo sahihi.
"Ninaipongeza Serikali kwa kutumia muda wa kutosha kuelimisha jamii umuhimu wa Sensa, makundi mbalimbali yamehamasisha Sensa ikiwemo, viongozi wa dini, siasa na hata viongozi wa mila, kila mmoja kwa nafasi yake amehakikisha, watanzania wanaingia kwenye Sensa wakiwa na taarifa sahihi huku wakitambua umuhimu wa kuhesabiwa" Amesema Mwenyekiti Zelothe
Zoezi la Sensa ya watu na Makazi linaendelea katika halmashauri ya Arusha,huku kukiwa na hali ya amani na utulivu, wakazi wa halmasahuri hiyo wakiwa nyumbani kusubiri Makarani wa Sensa kufika kwenye kaya zao.
HAKIKISHA UMEHESABIWA✍✍
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.