Na. Elinipa Lupembe.
Kufuatia sera ya Serikali ya awamu ya tano ya kutoa elimu bila malipo, kuanzia shule ya awali mpaka kidato cha nne, sera inayoenda sambamba na mkakati thabiti wa uboreshaji wa miundombinu ya shule, kupitia miradi yake ya Lipa kutokana na Matokeo 'EP4R', imeanza kujenga maktaba kwenye shule za sekondari za kata nchini.
Halmashauri ya Arusha, ni miongoni mwa halmashauri zilizonufaika na neema hiyo, kwa kupewa kiasi cha shilingi milioni 100, kwa ajili ya ujenzi wa maktaba katika shule zake mbili za sekondari za Mwandet na Mlangarini.
Akizungumzia adhma ya serikali ya awamu ya tano, Mkurugenzi mtendaji, halmashauri hiyo, Dkt. Wilson Mahera, amesema kuwa, katika kuboresha miundombinu ya shule, serikali imekwenda mbali zaidi kwa kuanza kujenga maktaba kwenye shule za sekondari za kata, ambazo hapo awali shule hizo hazikuwa na maktaba.
Amesema kuwa, maktaba ni sehemu muhimu katika mchakato mzima wa ufundishaji na kujifunza, unaompa fursa mwanafunzi kujisomea zaidi akiwa mwenyewe na kujipatia maarifa zaidi, kwa yale aliyofundishwa na mwalimu akiwa darasani.
"Maktaba ni muhimu katika shule, inakuza taaluma na inamfanya mwanafunzi kujisomea kwa uhuru na kupata maarifa katika mawanda mapana zaidi, kwa kile alichofundishwa na mwalimu darasani, pamoja na kujifunza mambo mbalimbali ya kijamii" amesema mkurugenzi huyo
Wadau mbalimbali wa elimu wametoa maoni yao tofauti juu ya umuhimu wa ujenzi huo makta kwenye shule za kata, licha ya kuipongeza na kuishukuru serikali ya awamu ya tano, kwa kuwekeza fedha nyingi kwenye kuboresha miundombinu ya elimu, kutokana na ukweli kwamba mazingira bora ya kujifunzia, ni chachu ya mwanafunzi kujifunza na kumwezesha mwanafunzi kuwa na uwezo mkubwa wa kuelewa kile alichofundishwa.
Janeth Shayo mwalimu wa shule ya msingi Olchoki, halmashauri ya Arusha, amethibitisha kuwa, kuna tofauti kubwa ya kujifunza kati ya mwanafunzi aliye kwenye mazingira bora na vifaa, na yule anayejifunza kwenye mazingira duni yasiyo na vifaa.
Ameongeza kuwa uwepo wa mazingira bora na vifaa vya kujifunzia, hutoa msukumo chanya kwa mwanafunzi kujifunza tofauti na yule aliye kwenye mazingira duni kwani huwa na msukumo hafifu na wakati mwingine huwa hasi kabisa.
Naye mkuu wa shule ya sekondari Mlangarini, mwalimu Elisa Pallangyo, ameshukuru na kupongeza juhudi za serikali, za kuwekeza hasa kwenye shule changa, shule za kata ambazo zimeanza huku zikiwa, hazijitoshelezi hasa katika miundombinu yake.
Amesema kuwa, uwepo wa maktaba shuleni kwake, utawawezesha wanafunzi kuwa na muda wa kutosha wa kujisomea, na kwa utulivu zaidi kuliko wawapo madarasani, huku maktaba hiyo ikisaidia utunzaji rahisi na imara wa vitabu, tofauti na hapo awali ambapo kulikuwa na upotevu wa vitabu.
" Maktaba itawawezesha wanafunzi kupata muda zaidi wa kujisomea wenyewe na kwa utulivu, pamoja na urahisi wa upatikanaji wa vitabu unaoenda samvamba na utunzaji wa vitabu, ambao kwa sasa ni mgumu, kw kuwa vitabu vinapotea kwa urahisi" amesema mkuu huyo wa shule.
Aidha, ujenzi wa maktaba zote mbili uko kwenye hatua za boma huku ukiendelea kwa kasi na unategemewa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu wa Aprili na wanafunzi kuanza kupata huduma bora kwenye majengo hayo yote.
Awali, Halmashauri ya Arusha imepokea kiasi cha shilingi milioni 220, kutoka serikali kuu kupitia wizara ya Elimu na miradi ya EP4R, fedha ambazo milioni 110, zimetumika kujenga maktaba katika shule ya sekondari Mwandet na Mlangarini, kwa gharama ya shilingi milioni 50 kila mmoja, huku shilingi milioni 110 zikitumika kukarabati na kumalizia mabwalo ya chakula kwa shule zote mbili.
PICHA ZA MAJENGO YA MAKTABA HIZO
Muonekano wa jengo la Maktaba shule ya sekondari Mlangarini.
Muonekano wa jengo la Maktaba ya shule ya sekondari Mwandeti.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.