Kufuatia mpango mkakati wa Serikali ya awamu ya tano, wa kupambana na kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini, halmashauri ya Arusha kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, imejipanga kuanzisha klabu za watoto kwenye shule zake 20 za msingi na sekondari, kwa mwaka huu wa fedha 2019/2020.
Mkakati huo umewekwa wazi wakati wa mafunzo ya ufunguzi wa mradi huo, unaotegemea kutekelezwa na shirika la Center for Women and Children Development 'CWCD', kwa ufadhili wa shirika la Civil Society Foundation, uliowakutanisha watalamu wa halmashauri kuanzia ngazi ya kijiji, viongozi wa serikali na wawakilishi wa wananchi ikiwemo madiwani na wenyeviti wa vijiji na vitongoji, mafunzo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.
Mwezeshaji wa Mafunzo kutoka shirika la CWCD, Happy Josephat, amesema lengo la mradi huo kuanzisha klabu shuleni ni kuzuia ukatili dhidi ya watoto, kwa kuwajengea watoto uwezo wa kujitambua, kutambua haki na wajibu wao, kufahamu jukumu lao la kujilinda dhidi ya ukatili na uwezo wa kutoa taarifa kwa wakati.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajenga, uelewa wa pamoja kwa watalamu na viongozi wa jamii ili kushirikiana kwa pamoja kupambana na ukatili dhidi ya watoto.
Aidha ameeleza kuwa, shirika linajukumu la kuwajengea uwezo walimu, watakaowafundisha watoto hao, kwa usimamizi wa viongozi wote wa serikali na jamii ili kupambana na ukatili dhidi ya watoto.
Naye Mkurugenzi Mtendajim halmashauri ya Arusha, licha ya kulishukuru shirika hilo, ameahidi kutoa ushirikiano na kuwataka watalamu wa ngazi za kata na vijiji pamoja na walimu, kutumia fursa hiyo kuzuia ukatili wa watoto katika maeneo yao.
Ameongeza kuwa licha ya matukio hayo, kuanza kupungua kwa sasa, lakini bado kuna maeneo ambayo yanachangamoto, zinazotokana na mila na desturi, na kuitaka jamii kubadilika na kutokomeza mila hizo, zinazowadhalilisha watoto na wanawake kwa kuwakandamiza na kuwanyima haki zao za msingi.
Hata hivyo, viongozi walioshiriki mafunzo hayo, wamelalamikia mahakama na polisi, kushindwa kutoa haki kwa watoto waathirika wa ukatili na badala yake, watuhumiwa kuachiwa huru kwa madai ya kukosa ushahidi, na kuwaacha viongozi uhasama na familia za watuhumiwa.
Diwani wa kata ya Kiranyi, mheshimiwa Jombi Seneu, amethibitisha kuwa, viongozi wanajitahidi kupambana na ukatili katika maeneo yao, na kuwakamata watu wanaofanya vitendo, hivyo lakini bado sheria za polisi na mahaka zinapaswa kuangaliwa upya, kwa kuwapa nafasi watuhumiwa kudhaminiwa na kumaliza kesi hizo kwa mazungumzo mezani, matokeo yake viongozi na watu walioshiriki kumkamta mtuhumiwa kubaki na uhasama na familia ya mtuhumiwa.
"Viongozi na wananchi,tunamkamata mtuhumiwa na kumfikisha polisi, polisi anapewa dhamana, anakuja nyumbani anapata nafasi ya kukaa na ile familia wanazungumza, bado sheria ni kinzani, zinazopoteza au kuharibu ushahidi, pindi mtoto anapofanyiwa ukatili, zinapaswa kuangaliwa upya" amesema Diwani Seneu.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, jamii imeelekeza lawama kwa wazazi, kwa madai kuwa licha ya juhudi za serikali, wadau, viongozi na jamii kunia mamoja, bado wazazi wako nyuma katika mapa,bano ya kutokomeza ukatili dhidi ya watoto, kwa kukubali kumalizana na watuhumiwa, kwa kushiriki kuficha watuhumiwa wanaowapa mimba watoto wa kike, kuwaozesha watoto, kuwafanyia tohara watoto wa kike, kuficha siri za matukio ya ubakaji na ulawiti yanayofanyika ndani ya familia zao.
Hindu Mbwego, mkurugenzi wa shirika la CWCD amethibitisha kuwa, bado wazazi wameshindwa kutekeleza majukumu yao katika kutokomeza ukatili dhidi ya watoto, licha ya serikali na jamii kuungana tupambana na wahalifu wanafanya vitendo vya ukatili kwa watoto.
Amefafanua kuwa, jamii inamkamata mtuhumiwa na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria, kukiwa na yshahidi wa kutosha, lakini wazazi wanakubali kuzungumza na mtuhumiwa, matokeo yake wanamfundisha mtoto kubadilisha ushahidi, pengine wanamuhamisha na wakati mwingine kumzuia au kutokumpeleka mtoto mahakamani wakati wa kesi.
Hata hivyo Hindu ameeleza kuwa, matukio mengi ya ukatili kwa watoto yanafanyika nyumbani ndani ya familia, hivyo watuhumiwa wengi ni ndugu na jamaa, hivyo wazazi kushindwa kusimamia wajibu wao kwa kumtetea mtoto na badala yake, husimamia mahusiano yao na watuhumiwa ndani ya familia zao.
" Wazazi wanashirikiana na watuhumiwa, ama kwa kupewa fedha au kwa kuwa watuhumiwa ni member wa familia, pengine ni baba, mjomba ama babu, wazazi wanashindwa kusimama kumtetea mtoto wao kwa kuwakinga ndugu na jamaa zao na kuhofia kujenga uhasama kwa ndugu zao."
Awali mradi huo wa mwaka mmoja unategememea kutekelezwa kwenye shule 30 kwenye kata za Bangata, Ilboru, Kiranyi, Moivo, Oloirien, Olturoto na Tarakwa, ikiwa shule 20 za msingi na 10 za Serikali.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.