Na. Elinipa Lupembe.
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF, umeendelea kuimarisha, maisha ya wakazi wa halmashauri ya Arusha kisekta, tangu TASAF awamu ya III kupitia miradi ya OPEC, ilipoanza kutekelezwa mwezi Juni mwaka 2013.
Wananchi wa halmashauri hiyo, wameemdelea kunufaika katika sekta za Elimu, Afya, Kilimo na Mifugo, miundombinu ya barabara, uwezeshaji wananchi kiuchumi, huku kaya masikini zikiendelea kupokea fedha za ruzuku, kupitia utekelezaji wa mradi wa Uhawilishaji fedha kwa Kaya Masikini.
Kwa kipindi cha robo ya pili, ya mwaka huu wa fedha 2019/2020, halmashauri ya Arusha, imepokea kiasi cha shilingi milioni 216.98, kwa ajili ya kutekeleza miradi mitatu, katika sekta ya Elimu na Miundombinu ya barabara.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, ofisini kwake, Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Alvera Ndabagoye, amethibitisha halmashauri yake, kupokea kiasi hicho cha fedha, kilichoelekezwa kutekeleza miradi mitatu, ikiwemo ujenzi wa Kivuko cha Laroi kata ya Laroi, ujenzi wa nyumba mbili za walimu zenye sehemu mbili (2 in1), nyumba zenye uwezo wa kuishi familia mbili kwa kila nyumba, kwenye shule ya msingi Lemuguru kata ya Matevesi na shule ya msingi Losikito kata ya Mwandeti.
Aidha mkurugenzi Alvera, amefafanua kuwa, halmashauri imejipanga vema kutekeleza miradi hiyo kwa wakati, na hasa kwa kuzingatia ubora unaoendana na thamani ya fedha zilizoletwa, lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wake, wanapata huduma bora kupitia miradi hiyo, kama ilivyokusudiwa na Serikali ya awamu ya tano.
Aidha Mkurugenzi huyo, amewataka wananchi wa maeneo wanayonufaika na miradi hiyo, kujitoa kuchangia nguvu kazi ya asilimia 10, kama miongozo ya miradi ya TASAF inavyoelekeza, ili utekelezaji wa miradi hiyo uende kwa kasi na kukamilika kwa wakati, zaidi waweze kupata miradi mingine zaidi.
"Katika miradi hii, wananchi wanapaswa kujitolea nguvu kazi kwa asilimia 10, hivyo niwaombe wananchi wangu wa Laroi, Lemuguru na Losikito, kujitolea nguvu kazi hiyo, ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati, na Serikali iweze kutuletea miradi mingine zaidi, kwa faida yetu wenyewe" amesisitiza Mkurugenzi huyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mratibu wa TASAF halmashauri ya Arusha, Kabula Sukwa, amefafanua kuwa, tayari mchakato wa kupata wakandarasi wa kutekeleza miradi hiyo uko hatua za awali, na mara baada ya kukamilika hatua zote, miradi itaanza kutekelezwa, na kuongeza kuwa miradi yote hiyo, inategemewa kukamilika ndani ya mwaka huu wa fedha wa 2019/2020.
Hata hiyo, Kabula amezitaja gharama za kila mradi ni pamoja na ujenzi wa nyumba mbili za walimu zenye sehemu mbili (2 in 1) zitakazogharimu kiasi shilingi milioni 144.58 huku kila nyumba ikigharimu shilingi milioni 72.29 na mradi wa ujenzi wa kivuko cha Laroi ukigharimu kiasi cha shilingi milioni 72.38 na kufanya gharama za miradi yote mitatu kuwa ni shilingi milioni 216.98
Jumla ya vijiji 45 vya halmashauri ya Arusha, vinanufaika na miradi ya TASAF awamu ya tatu, kupitia miradi yake ya OPEC, huku takribani kaya 9045 zikinufaika mradi wa Uhawilishaji fedha kwa kaya masikini.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.