Na Elinipa Lupembe.
Mtalamu ufuatiliaji kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF makao makuu, Judith Masika, amewasilisha utaratibu na maelekezo ya Serikali kupitia TASAF, wa kuanza mchakato maalumu kuwaondoa kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini, walengwa walioboreka kutokana na mpango huo na kukidhi vigezo vya kuweza kujitegemea, pamoja na kuanza malipo kupitia mfumo wa kielektroniki na kuondoa malipo ya fedha taslimu.
Mratibu huyo, amewalezea Waheshimiwa Madiwani wakati wa mkutano wa Baraza la Kata, uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya Arusha kuwa, kutakuwa na zoezi maalum la kuwaondoa walengwa ambao wamekidhi vigezo kwa kuwa tayari wamekuwa na uwezo wa kuanzisha miradi inayowawezesha kujikimu kimaisha ili nafasi hizo zichukuliwe na walengwa wenye sifa ambao hawako kwenye mpango na wanakidhi vigezo vya kuingizwa kwenye mpango huo wa kunusuru kaya masikini.
"Zoezi hili litahusisha walengwa wa TASAF ambao tayari wameweza kujikimu kimaisha kwa kuanzisha miradi ambayo inawawezesha kupata mahitaji yao muhimu ya kimaisha na kukidhi vigezo vya kutokuwa kaya masikini tena, pamoja na baadhi ya walengwa kuingizwa kwenye mpango wakiwa hawana sifa, kwa kuwa wanauwezo na tunawafahamu kwa kuwa tunaishi nao katika maeneo yetu" Amesisitiza Judith
Aidha amelezea mabadiliko ya utaratibu wa serikali kupitia TASAF, wa kuwasajili walengwa kwenye mfumo ili waweze kulipwa ruzuku ya fedha kwa njia ya kielektroniki kupitia mitandao ya simu, benki na mawakala wa mitandao ya simu na kuachana na utaratibu uliopo wa kulipa fedha taslimu.
Amefafanua kuwa utaratibu wa kuwaondoa walengwa hao, utafanyika kupitia mkutano mkuu mkuu wa kijiji, na utahusisha walengwa wote walio kwenye mpango, kwa kuwasajili kwenye mfumo kupitia vitambulisho vyao vya Taifa (NIDA) na kusajili namba zao za simu na kwa walengwa wasio na simu wala akaunti za benki watatumia mawakala wa simu waliopo kwenye maeneo yao
Hata hivyo waheshimiwa madiwani walibainisha changamoto za maeneo yasiyo na mtandao ya simu, wazee wasio na simu na wale wasiojua kusoma na kuandika, wagonjwa na kaya ambazo zinaongozwa na watoto wasio na wazazi.
Mratibu huyo amefafanua kuwa, kwa walengwa ambao ni wazee sana, wasiojua kusoma na kuandika, wagonjwa, na kaya zinazoongozwa na watoto zitahudumiwa kupitia mawakala ambao wanasimamiwa na uongozi wa TASAF pamoja na program ya wasimamizi wa walengwa watakaochaguliwa kutoka kwenye jamii husika.
Aidha ameweka wazi faida za malipo kwa njia ya kielekroniki ni pamoja na usalama wa fedha za walengwa na kuondoa wizi na upotevu wa fedha, hali za udanganyifu, pamoja na kuwapa fursa walengwa kufanya maamuzi sahihi ya matumizi ya fedha, huku ikiokoa muda kwa walengwa badala ya kupanga foleni kusubiri fedha,watatumia muda huo kufanya shughuli nyingine za maendeleo za kuwaingizia kipato.
Awali, amewataka madiwani hao, kushirikiana na wananchi, uongozi wa vijiji katika maeneo yao, na kuwa mabalozi wazuri kwa kuweleimisha wananchi kutambua umuhimu wa zoezi hilo, lenye manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
ARUSHA DC
KAZI INAENDELEA
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.