Na.Elinipa Lupembe.
Wananchi halmashauri ya Arusha wametakiwa kuunga mkono juhudi za serikali yao, kwa kutumia vituo vya afya vinavyojengwa katika maeneo yao kwa kujiunga kwenye mfuko wa Bima ya Afya - CHF iliyoboreshwa, ili kurahisihsa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo hivyo vya kutolea huduma za afya.
Rai hiyo imetolewa na wajumbe wa Kamati ya Siasa wilaya ya Arumeru wakati walipofanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika halmashauri ya Arusha, ikiwa na lengo la kukagua utelelezaji wa Ilani ya Chama cah Mapinduzi kwa vitendo, kuelekea maadhimisho ya miaka 44 tangu kuzaliwa kwa CCM Februari, 1977.
Wajumbe hao wamesema kuwa serikali ya awamu ya tano imejikita katika kutatua kero za wananchi hususani katika sekta ya afya, kwa kujenga zahanati na vituo vya afya, lengo likiwa ni kuwasogezea wananchi huduma za afya katika maeneo yao, sambamba na kurahisisha upatikanaji wa matibabu, pamoja na kupunguza vifo vya mama hasa kwa wananchi waishio vijijini.
Wakizungumza na wananchi wa kata ya Musa, wakati wakikagua maendeleo ya mradi wa Zahanati ya Musa uliyojengwa kwa fedha za EP4R, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Arusha, Steven Zelote, amewataka wanachi kuhakikisha kila kaya, inakuwa na kadi ya BIMA ya Afya - CHF iliyoboreshwa, ili kufikia malengo ya serikali ya kuwapatia wananchi huduma muhimu za afya katika maeneo yao, kwa kuwa tayari serikali, imejenga zahanati na vituo vya afya katika mmaeneo yao.
Mwenyekti Zelote amefafanua kuwa, serikali imetekeleza jukumu lake la kujenga zahanati na vituo vya afya katika maeneo ya vijijini, ni wajibu wa wananchi sasa kutumia zahanati hizo, kwa kutekeleza mpango wa kukata kadi za kadi za Bima ya Afya na kuwa na uhakika wa kjtibia pindi wanapougua, ili kwenda sambamba na lengo la serikali ya awamu ya tano, inayoongozwa na chama makini cha CCM, lengo la kuwahudumia wananchi wanyonge kwa gharama nafuu.
"Kwa miaka 44 ya CCM kuongoza serikali ya Tanzania, wananchi wamekuwa na imani na chama hicho, kutokana na mafanikio makubwa ya kimaendeleo hususani katika kufikisha huduma za afya vijijini, hii inaweka wazi kuwa CCM ni chama imara, chenye uongozi imara kinachoongoza serikali imara yenye kuwajali wananchi wote" amesisitiza Mwenyekiti Zelote.
Naye Emmanuel Memutiye, mkazi wa kijiji cha Oloitushula, amelalamikia uwepo wa changamoto za matumizi ya Kadi za Bima za Afya, pindi inapomaliza muda wake, na kusababisha wagonjwa kukosa matibau kutokana na kadi hizo kumalizika muda wake.
Hata hivyo, kwa kujibu changamoto hizo, Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Arusha, Saad Mtambule, amewataka wananchi kuhakikisha wanafahamu muda wa mwisho wa matumizi ya kadi zao, na kuandaa mapema utaratibu wa kuzihuisha kadi hizo kabla ya kumalizika kwa muda wa matumizi ya kadi hizo.
"Ni vema kila mwenye kadi ya BIMA kufahamu muda wa kumalizika kwa kadi yake, na kujiandaa kuzihuisha 'kurenew' kabla ya muda wa mwisho wa matumizi yake, ili kuepusha changamoto za kushindwa kupata matibabu pindi mwanakaya anapougua, kwa kuwa kadi hizo zimeingizwa kwenye mfumo ambao ikiisha muda wake haiwezi kutumika, mfumo unaikataa" amesema Mkurugenzi Mtambule.
Awali wananchi wa kata ya Musa wamethibitisha, mafanikio makubwa ya ujenzi wa zahanati hiyo ya Musa, kwamba uwepo wa zahanati hiyo, umeleta mafanikio makubwa kwa wananchi wa Musa hasa wanawake na watoto, kutokana na ukweli kwamba kumeokoa na kupunguza vifo vya wanawake na watoto wakati wa kujifungua pamoja na kuongeza kasi ya wajawazito na watoto kuhudhuria kliniki kwa wakati.
Asnath Simoni mhudumu wa afya ngazi ya Jamii, amethibitisha kuwa, kumekuwa na mwamko mkubwa wa wajawazito kuhudhuria kliniki pamoja na kujifungulia kwanye zahanati, tofauti na hapo awali, wajawazito walikuwa hawahudhurii kliniki na kujifungulia nyumbani, jambo ambalo lilihatarisha afya na maisha ya wajawazito na watoto.
Ziara hiyo ya Kamati ya Siasa wilaya ya Arumeru, imefanikiwa kukagua jumla ya miradi 5 katika sekta ya afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara, ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020/2025, ikiwa ni muendelezo wa shughuli za Chama za kuelekea maadhimisho ya sikukuu za miaka 44 tangu kuzaliwa chama hicho, zitakazofanyika tarehe 06.02.2021.
PIICHA ZA MATUKIO YA UKAGUZI WA MIRADI ILIYOTEMBELEWA NA KAMATI YA SIASA WILAYA YA ARUMERU.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.