Kufuatia tukio la ajali ya kutitia kwa choo katika shule ya msingi seliani, kata ya Kimnyaki, Halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru mkuu wa wilaya hiyo Mheshimiwa Jerry Muro, ameendesha harambee ili kupata fedha za ujenzi wa choo kipya na cha kisasa.
Katika zoezi hilo Mh.Muro amechangia kiasi cha shilingi laki tano na kuungwa mkono na wananchi wa eneo hilo kuchangia fedha na kufanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi milioni moja na kuwezesha ujenzi wa choo hicho kuanza mara moja siku ya Jumatatu ijayo na wanafunzi waweze kupata huduma hiyo.
Mkuu huyo wa wilaya amemuagiza mkurugenzi mtendaji, halmashauri ya Arusha, kuanza mchakato wa dharura wa kupata vifaa vya ujenzi ikiwemo matofali na saruji kwa ajili ya kuanza ujenzi wa choo hicho na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya Jumatatu kwa ajili ya kujitolea kushiriki shughuli za ujenzi huo kwa hali na mali.
“Tukio hili ni la kwetu sote niwaombe wananchi kuwa watulivu, serikali yenu itashirikiana nanyi kuhakikisha choo kinajengwa na watoto wetu wataendelea na masomo yao kama kawaida”. Alisema Muro.
Wakati huo huo, Mh. Muro ameuomba uongozi wa kanisa la KKKT, Usharika wa Seliani kuwaruhusu wanafunzi kutumia choo cha kanisa hilo, kwa kipindi cha wiki moja ambacho serikali na wananchi wanapolishughulikia ujenzi wa choo hicho.
Akitoa taarifa ya ajali hiyo, mwakilishi wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, Sajenti Isaac Mollel, amesema kuwa, wamefanikiwa kumuokoa mwanafunzi mmoja wa darasa la kwanza Emanuel Zakaria (7) aliyekuwa chooni wakati wa tukio hilo, na kukimbizwa hospitali ya Seliani Ngaramtoni kwaajili ya matibabu.
Hata hivyo kwa mujibu wa Dkt. Mfawidhi hospitali ya Selian, mtoto huyo hakupata athari kubwa na anaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo, Samweli Mollel ameelezea chanzo cha ajalo hiyo, ni kutokana na miundo mbinu ya choo hicho, kuwa ya ya zamani iliyojengwa miaka mingi iliyopita, licha ya choo hicho kuwa na matundu machache kwa kulinganisha na idadi ya wanafunzi.
Mollel amethibitisha ushiriki wa wananchi wa kijiji hicho kwa serikali, katika ujenzi wa choo cha kisasa, chenye kujengwa shimo nje ili kuepuka madhara mengine kama hayo kutokea tena.
“Choo kilijengwa kizamani lakini kwa sasa tutahakikisha tunajenga choo bora cha kisasa, ambacho shimo lake litakuwa nje tofauti na la awali ili watoto wetu wasisumbuke tena” Amesisitiza Mwenyekiti huyo.
Tukio la kutitia kwa choo cha wanafunzi wa shule ya msingi Seliani, lilitokea majira ya saa tatu na nusu asubuhi, huku chanzo kikuu kikielezwa kuwa ni miundombinu chakavu ya choo hicho baada ya kutumika kwa muda mrefu na tayari wananchi wameshaanza kuchanga fedha kwaajili ya ujenzi wa choo kipya.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.