Na Elinipa Lupembe
Wanufaika wa mikopo isiyo na riba ya asilimia 10 ya mapato ya ndani inayotolewa na halmashauri kwa vikundi vya vijana, kina mama na walemavu, wametakiwa kufanya shughuli za uzalishaji zenye tija na zitakazoleta faida ili kupata faida na kumudu kurejesha mikopo hiyo.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Arusha, Angela Mvaa wakati walipokutana na wanavikundi hao kwaajili ya kusaini, mikataba ya kupokea fedha hizo, fedha ambazo zitarejesha kwa kipindi cha mwaka mmoja, katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.
Afisa Maendeleo huyo amebainisha kuwa ni vema kila kikundi kujikita kwenye shughuli za mradi ambao mmewasilisha kwenye andiko na kusimamia mradi huo ili uweze kuleta faida kwa manufaa ya familia na kurejesha deni pia.
Aidha amesema kuwa, ni muhimu kila mwanakikundi kutambua masharti ya mkopo unaotolewa na Serikali ya Awamu ya sita na kuwajibika ipasavyo kufanya shughuli za miradi iliyokusudiwa ili fedha hizo ziweze kurudishwa kwa wakati na kusisitiza utunzaji wa kumbukumbu za matumizi yote ya fedha ili kuepuka upotevu wa fedha za Serikali.
“Mikopo hii inatolewa kwa watu waliokidhi vigezo kulingana na kiasi cha fedha kilichopo na si vinginevyo, ninyi mna sifa na mmekidhi vigezo vya kupata mkopo huu, niwaombe kuepuka matumizi yoyote yasiyo ya lazima ili muweze kufikia malengo yenu na kurejesha fedha hizo kwa wakati.” Alisisitiza Mvaa.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii dawati la vijana halmashauri ya Arusha, Ahadi Mlay amesema kuwa lengo la Serikali kutoa mikopo hiyo isiyo na ribariba, walemavu, vikundi vya vijana na akinamama ni kutoa fursa kwa jamii kuinuka kiuchumi kupitia shughuli mbalimbli za uzalishaji ikiwa ni pamoja na kuzakuza ajira hasa kwa vijana ambao wanapitia changamoto ya kukosa mitaji ya kuanzisha biashara.
“Fedha hizi sio kwa ajili ya kugawana kwa kila mwanakikundi na kila mtu kufanya mradi anaotaka bali ni kwaajili ya kufanya mradi uliokusudiwa na wanakikundi wote kwa pamoja na faida itakayopatikana ndiyo inapaswa kugawanywa kwa kila mwanakundi.” Ameweka wazi Mlay.
Hata hivyo wanufaika hao wameishukuru Serikali ya Awamu ya sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali, wananchi wake na kuwapatia fursa nyingi za kujikwamua kiuchumi pamoja na kuzalisha ajira kwa watanzania waliokuwa wamekata tamaa ya kujiendeleza, kiuchumi kutokana na kukosa mitaji ya kufanyia biashara.
“Matamanio yangu ni kukuza biashara yangu ya nafaka, matunda na mbogamboga na kuwekeza zaidi ili niweze kuwa mfanyabiashara mkubwa, ninaishukuru sana Serikali kwa kutupatia fursa hii addhimu na ninawashauri na watanzania wengine kuchangamkia fursa hii masharti yake siyo magumu na hakuna ubaguzi.” Alisema Michael Thomas ambaye ni mlemavu wa Kata ya Mateves, mara baada ya kusaini mkataba wa mkopo
Awali, halmashauri ya Arusha imetoa shilingi milioni 217 kwa vikundi 15 ambapo, fedha hizo zinatarajiwa kurejeshwa kwa kipindi cha ndani ya miaka mitatu.
ARUSHA DC
KaaiInaendelea ✍
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.