Na.Elinipa Lupembe
Wazabuni wa kukusanya takataka katika maeneo mbalimbali ya halmashauri ya Arusha,wilayani Arumeru, wametakiwa kutambua kuwa kazi wanayoifanya ni ya kutoa huduma bora na stahiki kwa jamii na si kujikita na kuweka mbele zaidi maslahi wanayoyapata.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha Dkt. Wilson Mahera, alipokutana na wazabuni hao ofisini kwake, mapema wiki hii kwa lengo la kujadili njia bora ya utoaji huduma pamoja na changamoto zinazoikabili sekta hiyo, hususani katika swala zima ukusanyaji wa taka.
Amesema kuwa, licha ya changamoto nyingi zinazokabili sekta hiyo bado halmashauri inathamini kazi ya huduma zinazotolewa na Wazabuni hao, kwa wananchi na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia kanuni, sharia na taratibu na kujikita zaidi kwenye makubaliano yaliyomo kwenye mikataba ya zabuni zao.
Aidha Mkurugenzi huyo amewataka wananchi wote wanaopata huduma ya uzoaji taka katika maeneo yao, kulipia huduma hiyo kulingana na bei elekezi zilizotolewa na kufafanuliwa katika sheria ndogo za kuimarisha Afya na Usafi wa mazingira za Halmashauri hiyo.
“Huduma ya uzoaji taka katika mitaa, inalipiwa si huduma ya bure, niwatake wananchi kutoa ushirikiano kwa Wazabuni wa uzoaji taka pamoja na kutunza taka hizo mpaka pale gari litakapokuja kuzibeba” amesema Mkurugenzi huyo.
Hata hivyo wazabuni hao walizitaja changamoto zinazowakabili katika kazi ya ukusanyaji taka ikiwa ni pamoja na mazingira magumu ya kazi kutokana na changamoto ya ufinyu wa barabara na njia za kungia kwenye baadhi ya mitaa, gharama kubwa za uendeshaji na kutokulipwa kwa wakati na kuthibitisha kuwa, endapo changamoto hizo zitafanyiwa kazi na kulipwa fedha zao kwa wakati itasaidia kutatua changamoto hizo, na kuwawezesha kuzoa taka kwa wakati katika maeneo husika.
Licha ya changamoto hizo za uendeshaji, wazabuni hao wamelalamikia, baadhi ya wanasiasa wanaowashawishi wananchi kutolipa fedha kwa ajili ya huduma ya uzoaji taka, jambo linalosababisha migogoro baina ya wananchi na wazabuni na kukwamisha jithada hizo za kazi zao.
Hata hivyo mkurugenzi Mahera ameahidi kuwa ofisi yake kupitia Idara ya Usafishaji na Mazingira, kushirikiana na wazabuni hao kuweka mazingira bora kuanzia ngazi ya kijiji, kata na halmashauri kwa ujumla kuhakikisha zoezi hilo la uzoaji taka linafanyika kwa usahihi bila kuonea upende wowote kwa kusimamimia sheria ndogo za kuimarisha Afya na usafi wa Mazingira.
Aidha amewaonya wanasiasa wanaowarubuni wananchi na kuwashawishi kugoma kulipia huduma ya takataka na kusisitiza kuwa suala la uzoaji taka na usafi wa mazingira ni suala mtambuka lisilohitaji siasa.
" Wananchi mnapaswa kutambua uzoaji taka katika maeneo yenu ni kulinda afya zenu, athari za kinyume na hapo ni mlipuko wa magonjwa, ambao husababisha vifo, acheni kuwafuata wanasiasa wamaowarubuni, ulipiaji taka upo kisheria hauhitaji siasa" amesisitiza Mkurugenzi Mahera
Awali, Sheria ndogo za usafi, kuimarisha Afya na usafi wa mazingira ya halmashauri ya Arusha ya mwaka 2010, kifungu nambari 29 kinaeleza wazi adhabu ya mtu yeyote atakaye kamatwa kwa kushindwa kulipa hela ya taka atatozwa faini ya shilling laki tatu 300,000 ua kufungwa miezi 12 au adhabu zote kwa pamoja.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.