Na Elinipa Lupembe
Wazee halmashauri ya Arusha wametakiwa kuamini kuwa uzee ni baraka kutoka kwa Mungu hivyo kuwa tayari kuzikubali changamoto za utu uzima kwa kujiweka imara katika kukabiliana nazo kwa kuwa ni sehemu ya maisha ya uzee.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Dkt. Ojung'u Salekwa, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani 2023, yaliyofanyika kijiji cha Nduruma kata ya Nduruma ambapo zaidi ya wazee 400 walikusanyika kuadhimisha siku hiyo muhimu kwao.
Amesema kuwa umri unaposogea mwili unaanza kudhoofu na kusababisha kukubiliwa na changamoto nyingi za kijamii na kiuchumi jambo ambalo linasababisha uzee kuonekana kama ni tatizo na kuwasihi wazee kuzikubali na kutambua kuwa changamoto hizo ni sehemu ya maisha ya utu uzima, zisiwakatishe tamaa na kuona kuwa uzee ni tatizo, bali kujiweka imara kukabiliana nazo.
"Niwatie moyo wazee wangu, licha ya changamoto zinazowakabili, tambueni kuwa serikali ya awamu ya sita inatambua na kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na wazee katika kulijenga Taifa la Tanzania, kwa kuweka mazingira ya kuwahudumia wazee katika sekta mbalimbali pamoja na kuunda mabaraza ya wazee yanayotoa fursa ya kuwakutanisha na kubadilishana uzoefu kuanzia ngazi ya kata, wilaya, mkoa na mpaka Taifa". Amesema Mwenyekiti Ojung'u
Hata hivyo wazee hao licha ya kuishukuru serikali kwa jitihada za kuwajali na kuwahudumia, wamebainisha kuwa bado kuna changamoto za upatikanaji wa Bima za afya, upatikanaji wa vitambulisho vya wazee, vitambulisho vya taifa (NIDA) pamoja na baadhi ya wazee kushindwa kujihudumia kutokana na hali duni za kiuchumi huku wakiiomba serikali kuwaingiza kwenye mpango wa TASAF.
Akisoma risala ya Baraza la wazee, Katibu wa Baraza la Wazee halmashauri ya Arusha, Mzee Julias Marasi amesema kuwa bado idadi kubwa ya wazee hawana vitambulisho muhimu ikiwemo vya Taifa na vya wazee hali inayowasababishia usumbufu mkubwa pindi wanapohitaji baadhi ya huduma kwenye ofisi za umaa na zile za binafsi na kuiomba serikali kushugulikia changamoto hizo ili wazee waendele kunufaika na matunda ya nchi hii.
Ameongeza kuwa wapo wazee ambao bado wana ngunvu hivyo ni vyema serikali ikaandaa mpango wa kuwawezesha kiuchumi kwa kuwapa mikopo isiyokuwa na riba kama yalivyo makundi mengine maalumu ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Awali Maadhimisho ya Siku ya Wazee yana lenga kuhamasisha jamii kuongeza uelewa wa juu ya masuala yanayohusu uzee na kuzeeka ikiwemo haki zao na upatikanaji wa huduma muhimu kwa wakati.
Kauli mbiu:"Udhibiti wa Wazee kwenye Dunia yenye mabadiliko"
ARUSHA DC NI YETU, TUSHIRIKIANE KUIJENGA
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.