Na Elinipa Lupembe
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama, amewataka wakurugenzi kutumia rasilimali watu walizonazo katika halmashauri badala ya kusubiri serikali kuajiri watumishi.
Waziri Jenista ameyasema hayo, wakati wa kikao kazi cha siku moja kilichowakutanisha watumishi wa wailaya ya Arumeru yenye halmashauri mbili za Arusha na Meru, kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya Meru.
Waziri ametoa rai hiyo mara baada ya wakurugenzi wa halmashauri hizo, kuwasilisha taarifa ya hali ya watumishi katika halmashauri hizo ikionyesha kuna upungufu wa watumishi katika kada za afya, walimu, manunuzi na wakaguzi wa Ndani kutokana na sababu mbalimbali.
Hata hivyo Waziri Jenista amewaagiza wakurugenzi, kutumia watumishi ambao tayari wako kwenye ajira kwa kuwaendeleza kitaaluma kulingana na uhitaji na baadaye kuwabadilishia kada ili kukidhi upungufu uliopo badala ya kusubiri serikali kuu kuajiri.
"Tengenezeni uwiano wa watumishi wetu, kuna kada ambazo kuna zidio la watumishi, watumieni hao kwa makubaliano ya kimaandishi, wekeni bajeti ya kuwaendeleza kitaaluma, halafu wabadilishieni kada, kwa kufanya hivyo tutapunguza hili tatizo lakini zaidi tutaipunguzia serikali mzigo wa kuwa na watumishi wanaolipwa kwa kufanya kazi kidogo" Amesisitiza Waziri Jenista.
Hata hivyo Waziri Jenista amewataka Maafisa Rasilimali watu, kusimamia haki za watumishi bila upendeleo, kwa kuhakikisha kila mtumishi anapata haki yake sawa na mwingine, huku akisisitiza kila mtumishi kutimiza wajibu wake katika kutekeleza majukumu aliyopangiwa na mwajiri.
"Serikali imewaamini na kuwapa jukumu la kuwasimamia watumishi, wapatieni haki zao, ili tufikie lengo la serikali la kuwahudumia wananchi, mtumishi asipopata haki yake hata utendaji wake wa kazi unakuwa wa kulegalega, tunahitaji watumishi wenye kufanyakazi kwa weledi wakiwa na imani na serikali yao iliyowaajiri" Amesisitiza Mheshimiwa Waziri
Aidha Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Mhandisi Richard Ruyango licha ya kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa ujio wake na somo alilolitoa kwa watumishi, ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo, maoni na ushauri kwa kuhakikisha halmashauri za wilaya ya Arumeru zinawahudumia watumishi kwa haki na usawa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.
"Mheshimiwa Waziri leo tumeongeza maarifa na uelewa mkubwa katika kutimiza wajibu na kutekeleza majuku ya kiutumishi, kwa maendeleo ya Taifa letu, umetukumbusha watumishi tuna deni kubwa kuwahudumia wananchi, tukuahidi hatutakuangusha wewe na mheshimiwa Rais, nikuahidi tutaendelea kushirikiana na Maafisa Utumishi, kuhakikisha tuna wasimamia watumishi kutekeleza majukumu yao na kufikia lengo la serikali la kuwahudumia wananchi" Amesisitiza Mkuu wa wilaya.
Naye Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu na Utawala, Halmashauri ya Arusha, Elizabeth Ngobei, amekiri kupokea maelekezo na kwenda kuyafanyia kazi kwa kuhakikisha watumishi wanatimiza wajibu wao na kuoata haki zao ili kuongeza tija na ufanisi katika kazi.
Awali Mheshimiwa Waziri, amefanya ziara ya siku moja katika wilaya ya Arumeru na kufanya kikao na Wakuu wa Ifara na Vitengo wa halmashauri za Arusha na Meru pamoja na watumishi wa halamshauri ya Meru.
ARUSHA DC
KaziInaendelea
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.