Halmashauri ya Arusha wilaya ya Arumeru, imejipanga kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto unaotokana na mila na desturi potofu zinazoendelezwa ndani ya jamii.
Mikakati hiyo imeanza kwa kuunda kamati ya ulinzi na usalama wa wanawake na mtoto ngazi ya halmashauri, kufuatia mwongozo wa serikali wa mpango wa kitaifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo, kaimu mkurugenzi halmashauri ya Arusha, ndugu Paulus Kessy, amesema kuwa halmashauri imeunda kamati hii kwa lengo la kuhakikisha ulinzi na usalama wa wanawake na watoto kwa kutokomeza mila na desturi zinazowakandamiza.
Ameongeza kuwa suala la mila na destruri lina changamoto nyingi, hivyo kamati hii ina kazi kubwa ya kuelemisha jamii juu ya athari ya mila hizo kandamizi kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria za serikali.
"Kamati inatakiwa kuwa na uhusiano chanya kati ya wazazi, walezi, watoto na jamii nzima, uhusiano wenye lengo la kuelimishana na kukemea mila potofu, uhusiano utakaowezesha halmashauri kufikia lengo la mwanamke na mtoto kupata haki " amesema Kaimu mkurugenzi
Aidha kaimu mkurugenzi Kessy ameweka wazi mikakati itakayotekelezwa na halmashauri hiyo ni pamoja na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa asilimia 50% ifikapo mwaka 2025 kwa jamii kujengewa uwezo wa kusimamia haki za wanawake na watoto.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii mkoa wa Arusha Theresia Costantine, ameainisha majukumu ya kamati hiyo ni pamoja na kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto pamoja na kushiriki katika utoaji huduma kwa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto utatekelezeka, endapo kamati itafanyakazi kwa ushirikiano kwa kumuweke na mtoto kwanza.
Hata hivyo Sumaiya Abdul (12) , mwenyekiti wa Baraza la watoto halmashauri ya Arusha ameonyesha kufurahishwa na uundaji wa baraza hilo kuongeza kuwa anaamini kupitia kamati hii watoto watapata haki zao za msingi.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.